CWT KUWAUNGANISHA WALIMU KUTATUA CHANGAMOTO

 

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma

CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) kimesema kitaendelea kuwafikia walimu wote nchini na kuwaunganisha pamoja ili kutambua changamoto zinazowakabili na kuzifikisha kwa Serikali kwa ajili ya kupata ufumbuzi.

Kaimu Katibu Mkuu wa CWT, Magesa Protas, alisema hayo wakati akizungumza kuhusu maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani, ambayo kilele chake kinatarajiwa kufanyika Oktoba 5, 2026.

Magesa alisema CWT itaendelea kushirikiana na walimu katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha changamoto zao zinabainishwa, kujadiliwa na kuwasilishwa kwa mamlaka husika kwa wakati.

“Tutahakikisha tunawafikia walimu wote nchini tunaungana na Serikali na walimu wote kuleta unafuu kwa walimu nchini,” amesema.

Amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha mshikamano miongoni mwa walimu na kuongeza ushiriki wao katika kushughulikia masuala yanayohusu maslahi, mazingira ya kazi na maendeleo ya taaluma ya ualimu.

Magesa alisema CWT pia itaendelea na mazungumzo na Serikali kuhusu madai na changamoto mbalimbali za kiutumishi zinazowakabili walimu, huku akisisitiza umuhimu wa masuala hayo kushughulikiwa kwa wakati.

Amesema miongoni mwa masuala yanayohitaji kupewa kipaumbele ni malipo ya fedha za likizo, kupanda madaraja na stahiki nyingine za walimu.

“Tunaiomba Serikali kuendelea kulipa madeni mbalimbali kwa wakati, ikiwemo malipo ya fedha za likizo, kupanda madaraja na stahiki nyingine za walimu,” alisema.

Pamoja na kuwasilisha changamoto hizo, Magesa aliipongeza Serikali kwa hatua zilizochukuliwa katika kutatua baadhi ya kero za walimu, ikiwemo masuala ya madaraja na kuboresha miundombinu ya elimu nchini.

“Tunaendelea kuipongeza Serikali kwa kuboresha miundombinu tunaomba yale mengine yanayohusu walimu wayafanyie kazi ili mwalimu afanye kazi katika mazingira mazuri,” alisema.

Amesema kumhudumia mwalimu ni sehemu muhimu ya kuwekeza katika elimu na maendeleo ya Taifa kwa kuwa walimu wana jukumu la kuandaa kizazi cha baadaye.

Aidha, CWT imeitaka Serikali kuhakikisha maboresho ya miundombinu yanaendana na mabadiliko yanayofanyika katika mfumo wa elimu, hususan wakati nchi ikiendelea na utekelezaji wa mitaala mipya.

Magesa amesema utekelezaji wa mitaala hiyo unahitaji mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia, hivyo shule zinapaswa kuwa na miundombinu inayokidhi mahitaji ya walimu na wanafunzi.

Amesema CWT itaendelea kusimamia taaluma ya ualimu, kulinda hadhi yake na kuwasilisha kwa Serikali mapendekezo yatakayosaidia kuboresha maslahi na mazingira ya kazi ya walimu.

Awali, Kaimu Mweka Hazina wa CWT, James Asagwile, ameiomba Katibu Mkuu wa chama hicho kushughulikia malalamiko mbalimbali yanayowakabili baadhi ya waajiriwa wa CWT, ikiwemo suala la mishahara.

Asagwile anesema baadhi ya waajiriwa wamekuwa wakilalamikia mishahara yao kubaki katika viwango vya muda mrefu, hivyo kuomba suala hilo liangaliwe upya.

Maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani mwaka huu yanafanyika huku CWT ikisisitiza umuhimu wa Serikali, walimu na wadau wengine wa elimu kushirikiana katika kuboresha mazingira ya kazi, maslahi ya walimu na ubora wa elimu nchini.