Makamu wa Rais Alivyowasili Misri Kuiwakilisha Tanzania Mkutano wa AU

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius John Ndejembi.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius John Ndejembi, amewasili jijini New Alamein nchini Misri, tayari kwa kuiwakilisha Tanzania katika Mkutano wa Nane wa Uratibu wa Katikati ya Mwaka wa Umoja wa Afrika, pamoja na mikutano mingine ya ngazi ya juu ya Jumuiya za Kiuchumi za Kikanda.

Mkutano huo unaofanyika kuanzia Oktoba 2, 2026, unafanyika chini ya kaulimbiu “Africa on the Land of El Alamein”, ukiwakutanisha viongozi wa juu wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika pamoja na wawakilishi wa taasisi mbalimbali za kimataifa na kikanda.

Makamu wa Rais amewasili kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Al Alamein, ambapo amepokelewa na Waziri wa Michezo na Vijana wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Mhe. Gohar Nabil, Balozi wa Tanzania nchini Misri, Mhe. Meja Jenerali Richard Makanzo, pamoja na maafisa mbalimbali kutoka Serikali za Tanzania na Misri.

Mara baada ya kuwasili, Mhe. Ndejembi amepokea taarifa kuhusu maandalizi ya ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo, unaolenga kujadili na kuratibu masuala muhimu yanayohusu maendeleo na ushirikiano wa Bara la Afrika.

Mkutano huo pia unatoa nafasi kwa viongozi kujadili vipaumbele mbalimbali vya maendeleo ya Afrika, ikiwemo masuala ya uchumi, amani, usalama na kuimarisha ushirikiano miongoni mwa mataifa ya Afrika.

Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo ni sehemu ya kuendeleza nafasi yake ndani ya Umoja wa Afrika na kuchangia katika mijadala inayolenga kusukuma mbele utekelezaji wa vipaumbele vya maendeleo ya Bara la Afrika.

Makamu wa Rais anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika mkutano huo, ikiwa ni mwendelezo wa ushiriki wa Tanzania katika majukwaa ya kikanda na kimataifa yanayojadili masuala yenye maslahi kwa Tanzania na Bara la Afrika kwa ujumla.