Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu, amefungua kikao cha Kamati Tendaji ya Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) kilichofanyika leo tarehe 3 Oktoba, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC).
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Spika Zungu amewakaribisha wajumbe hao jijini Arusha na kuwahakikishia kuwa maandalizi yote kuelekea Mkutano Mkuu wa IPU yamekamilika na kwamba Tanzania inajivunia kwa mkutano huu mkubwa wa kibunge duniani kufanyika hapa nchini na kwenda kujadiliana masuala mbalimbali yanayoikumba dunia.
Katika hotuba yake, Spika Zungu amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka mazingira wezeshi na utekelezaji madhubuti uliofanikisha maandalizi na uratibu wa mkutano huo mkubwa nchini.
Vilevile, amempongeza Rais wa IPU (ambaye pia ni Spika Mstaafu wa Bunge la Tanzania), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, kwa uongozi wake thabiti, imara na madhubuti katika kipindi chote cha miaka mitatu ya uongozi wake kwenye umoja huo.
Kabla ya kuhitimisha maelezo yake, Spika Zungu amewasihi wajumbe wote kutumia fursa hiyo kutembelea na kujionea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo jijini Arusha na kote nchini Tanzania.
Kikao hicho cha Kamati Tendaji kimeongozwa rasmi na Rais wa IPU, Mhe. Dkt. Tulia Ackson.
Kikao hicho cha Kamati Tendaji ya IPU ni maalum kuelekea kuanza kwa Mkutano wa 153 wa IPU kesho Oktoba 04, 2026 ambapo itawakutanisha washiriki 2,000 kutoka nchi wanachama 183 wa IPU wakiwemo Maspika, Makatibu, Wabunge na Maafisa mbalimbali.




