Mambo wachumba wanayosahau kabla ya ndoa, madaktari waonya
Dar es Salaam. Ndoa si ahadi ya kuishi pamoja tu, bali ni safari inayohitaji uwazi, uaminifu, uvumilivu na uwajibikaji kuhusu afya ya kila mmoja.
Katika jamii ambayo maandalizi ya ndoa mara nyingi huzingatia mavazi, sherehe na zawadi, wataalamu wa afya wanasisitiza umuhimu wa wanandoa kupima afya zao kabla ya kufunga ndoa, kwa lengo la kulinda afya zao na watoto watakaowapata.
Akizungumza na Mwananchi, Dk Sadam Kimanga amesema vipimo kabla ya ndoa ni njia ya kutambua mapema changamoto za kiafya na kuchukua hatua stahiki.
“Kwa ujumla, wanandoa wanapaswa kupima magonjwa yanayoweza kuambukizwa kwa njia ya ngono. Hata ikionekana mmoja ana ugonjwa, atibiwe kwanza ndipo waendelee. Kama ni ugonjwa usiopona, atatumia dawa za kufubaza,” amesema.
Amesema pia ni muhimu wanandoa kufahamu makundi yao ya damu, akieleza kuwa makundi makuu ni A, B, AB na O, ambayo yanaweza kuwa chanya (+) au hasi (-).
Kwa mujibu wa Dk Kimanga, changamoto inaweza kujitokeza iwapo mama ana kundi hasi huku baba akiwa na kundi chanya, hali inayoweza kuathiri ujauzito.
Amesema mwili wa mama unaweza kuitambua damu yenye tofauti kama kitu kigeni na kutengeneza kinga, jambo ambalo linaweza kuleta changamoto katika mimba zinazofuata.
“Kwa mimba ya kwanza, kama haitaharibika, mtoto anaweza kuzaliwa njiti, akiwa na uzito mdogo au kupata manjano baada ya kuzaliwa. Asipotibiwa, anaweza kufariki ndani ya siku 28,” amesema.
Amesema tatizo linaweza kuzuiwa kwa sindano maalumu zinazotolewa wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua, hivyo ni muhimu wanandoa kufahamu hali zao mapema.
Makamu Mkuu Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Padre Pio (PCOHAS), Dk Yassin Mussa, amesema vipimo havihusu makundi ya damu pekee, bali pia magonjwa ya kurithi kama selimundu.
“Mtoto anapozaliwa anachukua vinasaba kutoka kwa baba na mama. Ili apate selimundu, ni lazima wazazi wote wawili wawe na vinasaba vya selimundu,” amesema.
Dk Mussa, ambaye ni daktari bingwa wa magonjwa ya binadamu, amesema ni muhimu kupima ili kujilinda dhidi ya maradhi na kusaidia wanandoa kupanga familia.
Kwa upande wake, Dk Shita Samwel amesema mtoto hurithi asilimia 50 ya vinasaba kutoka kwa kila mzazi, hivyo vipimo vinaweza kusaidia kutambua uwezekano wa kupata baadhi ya magonjwa ya kurithi.
“Kwa sababu ya ubadilishanaji wa taarifa za kijenetiki, inaweza kutokea mtoto akapata selimundu. Pia yapo magonjwa ya kuambukiza kama VVU,” amesema.
Hamida Salum, mkazi wa Temeke jijini Dar es Salaam, amesema alijifunza umuhimu wa vipimo baada ya kupata ujauzito wake wa kwanza na kukumbwa na changamoto za kiafya.
“Awali sikuwa nafahamu. Nilijua ni mimba tu inanisumbua. Niliumwa sana na nililazwa kuanzia nilipokuwa na miezi miwili hadi miezi mitano. Baadaye nilikuwa nachomwa sindano za kuzuia mimba isitoke na nilipojifungua, mtoto alikuwa na manjano,” amesema.
Amesema baadaye alielezwa na daktari kuwa changamoto hiyo ilihusiana na makundi ya damu na kwamba, kabla ya kupata mtoto wake wa pili, alianza kupata sindano za kinga.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wamesema suala hilo bado halijapewa uzito unaostahili.
Shaibu Muddi amesema kabla ya kufunga ndoa alizingatia kupima VVU pekee, akisema hakufahamu umuhimu wa kupima makundi ya damu.
Peter Mzilai, mkazi wa Sakina, Arusha, amesema kwake msingi mkubwa wa ndoa ni upendo na kwamba hakuzingatia vipimo hivyo kabla ya ndoa.
Kwa upande wake, Wande Mayunga amesema kabla ya kuolewa alipima VVU pekee kwa sababu hakuwa na elimu kuhusu umuhimu wa kupima makundi ya damu.
“Baada ya kupata ujauzito ndipo tulipoelekezwa kuwa ni muhimu kupima makundi ya damu na kujua namna ya kukinga,” amesema.
Wataalamu hao wamesisitiza kuwa elimu zaidi inahitajika ili jamii ielewe umuhimu wa vipimo kabla ya ndoa, si kwa ajili ya kutafuta sababu ya kutofunga ndoa, bali kuwasaidia wenza kufanya uamuzi sahihi kuhusu afya, ujauzito na watoto watakaowapata.

