JWTZ kutoa matibabu bure | Mwananchi
Dodoma. Mamia ya Watanzania wanatarajiwa kunufaika na huduma za matibabu bure kutoka kwa madaktari bingwa wa majeshi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), katika hospitali na vituo vya afya mbalimbali nchini.
Huduma hizo zitatolewa kuanzia Agosti 26 hadi Septemba Mosi, 2026, wakati wa maadhimisho ya wiki ya ushirikiano wa Majeshi ya Nchi Wanachama wa EAC, yatakayofanyika nchini Tanzania kwa mara ya sita.
Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Utawala Jeshini, Brigedia Jenerali Agatha Katua, amesema hayo leo Jumatano, Agosti 19, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu maandalizi ya maadhimisho hayo.
Amesema madaktari bingwa kutoka Tanzania na nchi wanachama wa EAC watashiriki kutoa huduma kwa wananchi bila malipo, ikiwa ni sehemu ya shughuli za kijamii zinazoambatana na maadhimisho hayo.
“JWTZ inapenda kuujulisha umma wa Watanzania kuwa Majeshi ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yatashiriki maadhimisho haya ya sita. Kwa mara ya mwisho hapa kwetu ilikuwa mwaka 2022. Kwenye maadhimisho hayo Majeshi yatatoa huduma za kitabibu na tutakuwa na madaktari bingwa,” amesema.
Amesema nchi zitakazoshiriki kutoa huduma hizo ni Burundi, Somalia, Rwanda, Kenya, Uganda na mwenyeji Tanzania.
Amesema wananchi watakaofika katika hospitali na vituo vilivyopangwa watapata huduma hizo bila kulipia.
Hospitali zitakazotoa huduma
Brigedia Jenerali Katua amesema huduma hizo zitatolewa katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Arusha na Zanzibar.
Kwa Dar es Salaam, amesema vituo vitakavyotumika ni Hospitali ya Wilaya ya Ubungo, Hospitali ya Vijibweni na Kituo cha Afya Yombo Malawi.
Mkoani Pwani, huduma zitatolewa katika Hospitali Teule ya Rufaa Tumbi na Hospitali ya Bagamoyo, huku Zanzibar huduma hizo zikitolewa katika Hospitali ya Wilaya ya Mwerapongwe, Unguja, na Vitongojini, Pemba.
Mbali na matibabu, amesema maadhimisho hayo yatahusisha pia utoaji wa misaada ya kijamii, ukarabati wa vituo vya afya, vituo vya kulelea watoto yatima na magereza.
Amesema vituo vitakavyonufaika na ukarabati na misaada hiyo ni Kurasini, Mwandaiwa Orphanage Center iliyopo Bunju, Chanika Children Shelter, SOS Orphanage Centre Zanzibar na Kituo cha Afya Mapinduzi cha Dodoma.
Kwa upande wa magereza, amesema ukarabati utafanyika katika Gereza la Kisongo mkoani Arusha na Gereza la Segerea jijini Dar es Salaam.

