Skip to content
-
Subscribe to our newsletter & never miss our best posts. Subscribe Now!
Habarimpya

Habari Mpya Kilasiku

Habarimpya

Habari Mpya Kilasiku

  • Home
  • Sample Page
  • Home
  • Sample Page
Close

Search

  • https://www.facebook.com/
  • https://twitter.com/
  • https://t.me/
  • https://www.instagram.com/
  • https://youtube.com/
Subscribe
Habari

Kesi ya ugaidi mhadhiri UDOM, vigogo CWT zatupwa wiki ijayo

By admin
August 19, 2026 3 Min Read
Comments Off on Kesi ya ugaidi mhadhiri UDOM, vigogo CWT zatupwa wiki ijayo

Dodoma. Kesi ya ugaidi na uhujumu uchumi inayomkabili mhadhiri msaidizi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Melkizedeck Kaijage, imeahirishwa hadi Agosti 27, 2026, baada ya hakimu anayesikiliza shauri hilo kupata dharura na kushindwa kufika mahakamani.

Kaijage amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thurston Kombe leo Jumatano, Agosti 19, 2026, akikabiliwa na mashtaka ya ugaidi yanayoambatana na makosa ya uhujumu uchumi.

Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Francis Mwakifuna, ameiomba Mahakama kuahirisha shauri hilo akieleza kuwa Hakimu Zabibu Mpangule, anayesikiliza kesi hiyo, amepata dharura na hivyo hakuweza kufika mahakamani.



Baada ya maelezo hayo, Hakimu Kombe ameahirisha shauri hilo hadi Agosti 27, 2026, litakapotajwa tena.

Wakili wa utetezi, Godfrey Wasonga, amesema kesi hiyo ipo katika hatua za kuchukua maelezo ya awali kabla ya kupelekwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kusikilizwa.

“Mteja wangu anakabiliwa na mashtaka ya ugaidi yakienda sambamba na makosa ya uhujumu uchumi ambapo inadaiwa Julai 3, 2026, akiwa Chuo Kikuu cha Dodoma, alitishia kuchoma majengo yote ya umma pamoja na makazi ya polisi nchi nzima Tanzania Bara na Zanzibar, kinyume na Sheria ya Makosa ya Ugaidi,” amesema Wasonga.

Wasonga amesema kosa hilo halina dhamana, hivyo mshtakiwa anaendelea kushikiliwa mahabusu.

Katika shauri jingine lililotajwa mahakamani hapo, vigogo wanane wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wanaendelea kusota rumande katika kesi ya uhujumu uchumi na rushwa, huku upande wa Jamhuri ukieleza kuwa ushahidi wa kesi hiyo umekamilika na taarifa zake tayari zimepakiwa kwenye mfumo wa Mahakama.

Mwakifuna ameiambia Mahakama kuwa upande wa Jamhuri unasubiri Msajili wa Mahakama kupitia taarifa hizo na kujiridhisha kabla ya kuzishusha kutoka kwenye mfumo, hatua itakayowezesha washtakiwa kusomewa ushahidi wa tuhuma zinazowakabili.

“Taarifa zimeshawekwa kwenye mfumo wa Mahakama na kila mwenye uwezo wa kuufikia mfumo anaweza kuangalia. Msajili anaendelea kufuatilia na atakapojiridhisha ataishusha na kutoa nakala yake ambayo watuhumiwa watasomewa,” amesema Mwakifuna.

Mwendesha Mashtaka huyo ameiomba Mahakama itoe tarehe ya karibu ya kuendelea na shauri hilo wakati wakisubiri Msajili kukamilisha utaratibu wa kupitia taarifa hizo.

Hata hivyo, upande wa utetezi umepinga maelezo hayo na kuomba uthibitisho kwamba taarifa hizo kweli zimepakiwa kwenye mfumo wa Mahakama.

Mawakili hao wamesema hawaoni nyaraka hizo kwenye mfumo na kupendekeza, ikiwezekana, waambatane na upande wa Jamhuri kwenda kwa Msajili wa Mahakama ili kuthibitisha uwepo wa nyaraka hizo.

Vigogo hao walifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma Mei 25, 2026, na kusomewa jumla ya mashtaka 14 ya uhujumu uchumi na rushwa.

Hata hivyo, hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Washtakiwa kwenye kesi hiyo ni Leah Ulaya, Suleiman Ikomba, Maganga Joseph, Joseph Misalaba, Nashon Kidudu, Baraka Mbonalibha, Wambura Kihengu na kampuni ya Pyrite and Industries Company Limited.

Baada ya mabishano kati ya upande wa Jamhuri na utetezi kuhusu uwepo wa taarifa za ushahidi kwenye mfumo wa Mahakama, Hakimu Mkazi Mkuu, Thurston Kombe, ameahirisha shauri hilo hadi Ijumaa, Agosti 21, 2026, litakapotajwa tena.

Author

admin

Follow Me
Other Articles
Previous

DC HAI AENDELEA KUSIKILIZA KERO ZA WANANCHI, ATATUA MIGOGORO YA ARDHI

Next

Mambo wachumba wanayosahau kabla ya ndoa, madaktari waonya

Recent Posts

  • MATUKIO KATIKA PICHA MAZISHI YA MWL JOHN KIDAKULE
  • Mkakati wa kukabili uhaba wa maji na njaa, kuongeza tija ya kilimo
  • Mambo wachumba wanayosahau kabla ya ndoa, madaktari waonya
  • Kesi ya ugaidi mhadhiri UDOM, vigogo CWT zatupwa wiki ijayo
  • DC HAI AENDELEA KUSIKILIZA KERO ZA WANANCHI, ATATUA MIGOGORO YA ARDHI

Recent Comments

  1. A WordPress Commenter on Hello world!

Archives

  • August 2026

Categories

  • Habari
  • Magazeti
  • Michezo
Copyright 2026 — Habarimpya. All rights reserved. Blogsy WordPress Theme