DC SHAKA: MIILI YENU ISIWE KITEGA UCHUMI

Na Matukio Daima Media, Kilosa.

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, amewataka wakulima na wananchi wa Kata ya Magole kuacha kutumia madhara wanayopata katika migogoro ya wakulima na wafugaji kama njia ya kujipatia fedha.

Shaka amesema baadhi ya wananchi wamekuwa wakipokea malipo kutoka kwa watuhumiwa na baadaye kuacha kutoa ushahidi mahakamani dhidi ya vitendo hivyo.

Amesema hali hiyo inaweza kudhoofisha kesi na kuacha mazingira ya matukio ya ukatili kujirudia, hivyo amewataka wananchi kushirikiana na vyombo vya dola hadi hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya watuhumiwa.

Lakini wakati Shaka akitoa tahadhari hiyo, wakazi wa Magole wameibua changamoto nyingine inayohusiana na maisha yao ya kila siku ikiwemo upatikanaji wa ardhi ya kilimo na zahanati isiyo na huduma Rafiki.

Wananchi hao wameiomba Serikali kuwawezesha kupata maeneo ya kulima, hususan mashamba yaliyofutwa, wakisema ongezeko la watu limeongeza mahitaji ya ardhi kwa shughuli za kilimo.

Omary Saidi na Elia Chisongela ni miongoni mwa wakazi walioeleza hitaji hilo huku pia wakibainisha changamoto ya upatikanaji wa huduma za afya kuwa ni changamoto katika maeneo yao.

Kwa upande wake, Shaka amesema Serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya mtu yeyote anayechangia migogoro hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kutumia vyombo vya dola katika kushughulikia vitendo vya ukatili.

Mwisho