SERIKALI imezindua programu ya uwezeshaji mitaji ya Sh bilioni tano kwa kampuni changa za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), kwa lengo la kuzisaidia kukuza biashara, kuongeza ajira na kutengeneza suluhisho za kidijitali zinazochochea maendeleo ya uchumi.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, amesema hayo wakati wa uzinduzi wa programu ya uwezeshaji mitaji kwa kampuni changa za TEHAMA (STARS-UPS), akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wabunifu kutumia teknolojia kutatua changamoto katika sekta mbalimbali.
Amesema katika zama hizi za maendeleo ya teknolojia, ubunifu ni nyenzo muhimu katika kukuza uchumi, hivyo Serikali kupitia Tume ya TEHAMA imeendelea kuweka mazingira yanayowezesha kampuni changa kuanzisha, kuimarisha na kupanua biashara zao.
Kairuki amesema programu hiyo inalenga kuwapatia wajasiriamali wa TEHAMA mitaji itakayowawezesha kubadilisha mawazo bunifu kuwa bidhaa na huduma zenye thamani ya kiuchumi, huku utekelezaji wake ukifanyika kwa kushirikiana na Benki ya Azania.
Amefafanua kuwa mikopo hiyo itatolewa katika madaraja matatu, kuanzia Sh milioni moja hadi milioni 25, zaidi ya Sh milioni 25 hadi milioni 50, na zaidi ya Sh milioni 50 hadi milioni 100, kwa kuzingatia vigezo na masharti yatakayowekwa.
Amesema programu hiyo inalenga kampuni zinazotengeneza suluhisho za kidijitali katika sekta za fedha, kilimo, utalii, elimu, bima, usafirishaji na ugavi, pamoja na biashara mtandao, ili kuongeza matumizi ya teknolojia katika shughuli za kiuchumi.
Waziri huyo amesema mafanikio ya programu hayatapimwa kwa kiasi cha fedha kilichotolewa pekee, bali pia ukuaji wa kampuni zitakazonufaika, ajira zitakazozalishwa, ongezeko la mauzo na mapato, bidhaa na huduma mpya zitakazoingia sokoni, upanuzi wa masoko na urejeshaji wa mikopo.
Amesisitiza kuwa fedha hizo zinapaswa kutumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa ili kuwezesha kampuni kuongeza uzalishaji, kuimarisha biashara na kutafuta masoko ndani na nje ya Tanzania.
“Fedha hizi ni moto, hivyo mkazifanyie kazi kwa malengo mliyokusudia, mjenge biashara zenu, mtafute masoko na muimarishe nidhamu ya fedha,” amesema.
Kairuki aliwataka wabunifu na kampuni changa za TEHAMA kujisajili katika mifumo inayotambuliwa na Serikali ili kurahisisha upatikanaji wa huduma na fursa zinazotolewa kwa sekta hiyo.
Aidha, ameitaka Tume ya TEHAMA kukamilisha mwongozo wa utekelezaji wa programu hiyo na kuweka mfumo wa kufuatilia na kupima ukuaji wa kampuni zitakazonufaika, ili kuhakikisha uwezeshaji huo unaleta matokeo yanayopimika.
Amesema pia ni muhimu kwa wabunifu wa TEHAMA kuanzisha umoja rasmi utakaowawezesha kuwa na sauti ya pamoja na kurahisisha ushirikiano wao na Serikali pamoja na wadau wengine.
“Mpango huu ni muhimu kwa umma. Wale watakaopata mikopo wahakikishe wanaitumia kwa madhumuni yaliyokusudiwa ili wengine nao waweze kunufaika,” amesema.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Khamis Abdulla, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono na msukumo wake katika kuendeleza sekta ya mawasiliano na TEHAMA nchini.
Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya TEHAMA, Dkt. Henry Mwanyika, amesema kampuni changa zimekuwa zikikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa mitaji, huku baadhi ya benki zikisita kufadhili biashara hizo kutokana na hatari zinazohusishwa na uwekezaji katika kampuni changa.
Amewataka wanufaika kurejesha mikopo kwa wakati ili fedha hizo ziendelee kutumika kuwawezesha vijana wengine wenye mawazo bunifu kukuza biashara zao.
” Fedha hizo si ruzuku wala sadaka, bali ni mikopo inayopaswa kurejeshwa ili kuhakikisha programu hiyo inaendelea kutoa fursa kwa kampuni nyingine zinazohitaji mitaji, ” Amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Startup Association (TSA), Zahoro Muhaji, amesema programu hiyo inaonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuendeleza kampuni changa na kukuza sekta ya ubunifu nchini.
Alisema Sh bilioni tano zilizotengwa ni mwanzo muhimu katika kupanua wigo wa uwezeshaji wa kampuni changa, akibainisha kuwa awali fursa za ushindani wa ubunifu zilikuwa zikitoa zawadi zilizofikia Sh milioni 50.
Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Dkt. Godwill Wanga, alisema uwekezaji huo unalenga kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali kupitia utengenezaji wa bidhaa, viwanda vya kidijitali na maendeleo ya sekta mahiri.
Aliwataka wabunifu kuelekeza matumizi ya teknolojia katika sekta zote 21 za uchumi ili kuongeza mchango wa ubunifu katika uzalishaji, uundaji wa ajira na maendeleo ya Taifa.
