DC HAI AENDELEA KUSIKILIZA KERO ZA WANANCHI, ATATUA MIGOGORO YA ARDHI
Na Ashrack Miraji Kilimanjaro
Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Mhe. Hassan Bomboko, ameendelea na ziara zake katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi, ikiwemo migogoro ya ardhi inayowakabili baadhi ya wananchi.
Katika ziara hizo, Mhe. Bomboko amekuwa akikutana na wananchi, viongozi wa Serikali za mitaa pamoja na wadau mbalimbali ili kupata taarifa za changamoto zinazowakabili na kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi kwa mujibu wa sheria, taratibu na haki.
Miongoni mwa changamoto zinazojitokeza katika maeneo hayo ni migogoro inayohusu matumizi na umiliki wa ardhi, ambapo Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza umuhimu wa wahusika kufuata taratibu za kisheria katika kutatua tofauti zao badala ya kuchukua hatua zinazoweza kuongeza migogoro katika jamii.
Mhe. Bomboko amesema Serikali itaendelea kusikiliza wananchi na kushughulikia kero zao kwa wakati, akisisitiza kuwa viongozi wana wajibu wa kuwa karibu na wananchi ili kutambua changamoto zinazowakabili na kuzitatua kwa ushirikiano.
Aidha, amewataka wananchi kutumia fursa za mikutano na ziara za viongozi kutoa changamoto zao kwa uwazi, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kushirikiana na Serikali katika kulinda amani, utulivu na mshikamano katika jamii.
Ziara hizo zinaendelea kuwa sehemu ya jitihada za Serikali Wilaya ya Hai za kuimarisha huduma kwa wananchi, kusikiliza kero zao na kutatua migogoro mbalimbali kwa njia ya mazungumzo na kwa kuzingatia sheria, ili kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani na kutumia rasilimali zao kwa maendeleo.





