Skip to content
-
Subscribe to our newsletter & never miss our best posts. Subscribe Now!
Habarimpya

Habari Mpya Kilasiku

Habarimpya

Habari Mpya Kilasiku

  • Home
  • Sample Page
  • Home
  • Sample Page
Close

Search

  • https://www.facebook.com/
  • https://twitter.com/
  • https://t.me/
  • https://www.instagram.com/
  • https://youtube.com/
Subscribe
Habari

Sababu, suluhu kupanda kwa bei ya saruji

By admin
August 19, 2026 3 Min Read
Comments Off on Sababu, suluhu kupanda kwa bei ya saruji

Dar es Salaam. Baada ya Serikali kuwapa wazalishaji wa saruji hadi Agosti 28, 2026 kushusha bei na kuboresha upatikanaji wa bidhaa hiyo, wasambazaji wamesema kusimama kwa uzalishaji katika baadhi ya viwanda na kuongezeka kwa gharama za usafirishaji kumechangia kupanda kwa bei.



Kwa mujibu wa wasambazaji hao, baadhi ya viwanda vikubwa vimesimamisha uzalishaji kwa muda kwa ajili ya matengenezo ya mitambo, hali iliyosababisha mahitaji ya saruji kuzidi uwezo wa uzalishaji na kuongeza foleni za magari viwandani.

Wamesema kurejea kwa uzalishaji katika viwanda vilivyosimama ndilo suluhisho la msingi la kuongeza upatikanaji wa saruji, kupunguza foleni na hatimaye kurejesha bei katika viwango vya awali.

Agosti 18, 2026, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Waziri Rajab Salum, aliwaita wazalishaji wa saruji kwenye kikao cha dharura kujadili kupanda kwa bei na changamoto ya upatikanaji wa bidhaa hiyo.

Salum aliwapa wazalishaji hadi Agosti 28 kutekeleza hatua za kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa saruji pamoja na kushusha bei, akisema Serikali itaendelea kufuatilia utekelezaji kabla ya kuchukua hatua nyingine.

Katika kikao hicho, wazalishaji walieleza kuwa upungufu wa saruji umechangiwa na hitilafu za mitambo katika baadhi ya viwanda vikubwa vinavyozalisha klinka (malighafi muhimu katika utengenezaji wa saruji), pamoja na gharama za mafuta na usafirishaji.

Akizungumza na Mwananchi, Meneja Masoko wa Kampuni ya Usambazaji ya Jakonda Materials, John Kavishe amesema muda wa kusubiri saruji viwandani umeongezeka kutoka siku mbili au tatu hadi karibu wiki mbili.

“Awali, ukipeleka gari kiwandani, ndani ya siku mbili au tatu umepakia. Sasa ni hadi wiki mbili. Hii imetokea kuanzia miezi miwili iliyopita, Juni na kuna foleni kubwa ya kupata mzigo,” amesema.

Kavishe amesema ucheleweshaji huo umeongeza gharama kwa wafanyabiashara kwa kuwa malori hukaa muda mrefu yakisubiri kupakia mzigo.

“Fikiria mwenye lori ndani ya wiki mbili unamlipaje? Wakala akimpa wakala mwingine mzigo, naye anataka faida na anaongeza Sh500. Ukifika dukani inaongezwa Sh1,000 hadi kumfikia mlaji wa mwisho,” amesema.

Kavishe amesema mfuko wa Nyati uliokuwa ukiuzwa kwa Sh18,000 umefikia Sh19,267 kwa bei ya jumla katika baadhi ya maeneo, huku Njombe ukifika karibu Sh21,000 kwa rejareja.

Amesema baadhi ya wazalishaji wanauza mfuko mmoja kwa takribani Sh20,500 kwa mteja mmoja mmoja kabla ya gharama nyingine za usafirishaji na usambazaji.

Msambazaji mwingine wa VGK Company ambaye hakutaja jina, amesema upatikanaji wa saruji viwandani umekuwa mgumu, akisema gari lao limekaa wiki bila kupakia.

Uchunguzi wa Mwananchi umeonesha mfuko wa saruji wa kilo 50 Kibaha mkoani Pwani unauzwa kati ya Sh20,000 na Sh22,000, kutegemea eneo, chapa na gharama za usambazaji.

Agripina John wa Kibaha amesema hivi karibuni alinunua mfuko kwa Sh20,000 kutoka Sh16,500.

“Bei imepanda ghafla na kutuweka katika mazingira magumu sisi wa hali ya chini. Serikali isimamie suala hili ili bei ishuke,” amesema.

Mkazi wa Dar es Salaam, Kindamba Kindamba amesema kupanda kwa bei kumewafanya baadhi ya watu kusimamisha au kuchelewesha ujenzi.

Dereva wa ‘kenta’, Salum Mbegu, amesema tangu Julai biashara yake imekuwa ngumu kutokana na kupungua kwa shughuli za ujenzi.

Uchunguzi unaonesha tani moja ya saruji inauzwa kwa wastani wa Sh321,251 kabla ya VAT, kutoka takribani Sh300,000 Juni.

Kwa kuwa tani moja ni sawa na mifuko 20 ya kilo 50, bei hiyo ni karibu Sh16,063 kwa mfuko kabla ya VAT, au takribani Sh18,954 baada ya VAT.

Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), Dk Matiko Mturi amesema gharama za usafirishaji, mahitaji makubwa na uhaba katika baadhi ya maeneo ni miongoni mwa sababu za kupanda kwa bei.

Amesema bei ya wastani ya tani moja Dar es Salaam imeongezeka kwa takribani Sh21,000 tangu Juni, huku mfuko ukitoka kiwandani kwa karibu Sh18,900 ukiwa na VAT kabla ya gharama za mawakala na usafirishaji.

Julai 8, 2026, Mwananchi iliripoti kuwa baadhi ya wazalishaji waliongeza bei kwa Sh500 hadi Sh650 kwa mfuko kabla ya VAT, wakitaja gharama za uzalishaji, malighafi, usafirishaji, kodi na uendeshaji.

Wadau sasa wanaona kurejea kwa uzalishaji katika viwanda vilivyosimama kuwa hatua muhimu ya kuongeza upatikanaji na kupunguza bei ya saruji nchini.

Author

admin

Follow Me
Other Articles
Previous

MATUKIO KATIKA PICHA MAZISHI YA MWL JOHN KIDAKULE

Next

CCM WAAGIZA KUFANYIKA UKARABATI WA SAKAFU BWENI LA ANNE MAKINDA SEKONDARI NJOMBE

Recent Posts

  • UNDP: Vyuo geuzeni tafiti kuwa biashara kutengeneza ajira
  • Kibaha yaimarisha upimaji ardhi kupunguza migogoro
  • Aliyembaka mtoto wa mwaka mmoja akwama rufaa, ahukumiwa jela maisha
  • JWTZ kutoa matibabu bure | Mwananchi
  • CCM WAAGIZA KUFANYIKA UKARABATI WA SAKAFU BWENI LA ANNE MAKINDA SEKONDARI NJOMBE

Recent Comments

  1. A WordPress Commenter on Hello world!

Archives

  • August 2026

Categories

  • Habari
  • Magazeti
  • Michezo
Copyright 2026 — Habarimpya. All rights reserved. Blogsy WordPress Theme