Wamiliki miundombinu muhimu ya Tehama watakiwa kuisajili
Dar es Salaam. Serikali imewataka wamiliki na waendeshaji wa miundombinu muhimu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kukamilisha usajili wake kabla ya Desemba 19, 2026, ikieleza kuwa hatua hiyo ni kuilinda dhidi ya mashambulizi ya mtandao, hitilafu na majanga.
Miundombinu hiyo ni ile inayojumuisha mali, vifaa, mifumo ya kompyuta na mitandao inayoshikika na isiyoshikika ambayo ina umuhimu kiasi kwamba ikishindwa kufanya kazi inaweza kusababisha madhara kwa usalama, uchumi na jamii.
Hatua hiyo inalenga kuweka msisitizo katika kutambua na kulinda miundombinu muhimu ya Tehama kutokana na kuongezeka kwa vitisho vinavyoweza kuvuruga huduma zinazotegemea mifumo ya kidijitali.
Hayo yameelezwa leo Jumatano Agosti 19,2026 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki ambaye ameeleza kuwa Serikali imebainisha miundombinu muhimu ya Tehama katika sekta mbalimbali ambayo inapaswa kusajiliwa ili iweze kupata ulinzi wa kisheria.
Hatua hiyo inatekelezwa kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandao Namba 14 ya mwaka 2015, hususan Kifungu cha 28(1), kinachompa waziri mwenye dhamana ya mawasiliano mamlaka ya kutangaza miundombinu muhimu ya Tehama.
Kwa mujibu wa Waziri Kairuki, sekta zenye miundombinu hiyo ni pamoja na habari na mawasiliano, fedha na benki, maji, afya, madini, usafirishaji, chakula na kilimo, ujenzi, uchumi wa buluu, mazingira, viwanda, ulinzi, anga, ardhi na elimu.
“Ni lazima kwanza itambuliwe kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa kisheria. Ulinzi wa miundombinu hiyo unalenga kuhakikisha inabaki salama, inapatikana na inafanya kazi kwa uhakika hata wakati kunapotokea mashambulizi ya mtandao, hitilafu au majanga,” amesema.
Kairuki amesema uharibifu wa miundombinu hiyo si jambo linaloweza kuchukuliwa kirahisi, kwa kuwa linaweza kusababisha madhara ya kiusalama na kiuchumi.
Kifungu cha 29 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 kinaweka adhabu ya faini isiyopungua Sh100 milioni au mara tatu ya hasara iliyosababishwa, kifungo kisichopungua miaka mitano au adhabu zote kwa pamoja.
“Kwa yeyote atakayebainika kutenda kosa la uharibifu kwa miundombinu muhimu ya Tehama, kwa mujibu wa Kifungu cha 29 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, mhusika atapata adhabu ya kulipa faini isiyopungua Sh100 milioni au mara tatu ya hasara iliyosababishwa au kifungo kisichopungua miaka mitano au vyote kwa pamoja,” amesema Kairuki.
Pamoja na tangazo kwa umma kuhusu usajili huo lililotolewa Juni 19,206 amesema wizara imeandaa miongozo mitano itakayosaidia wamiliki na waendeshaji wa miundombinu muhimu ya Tehama kuelewa wajibu wao katika kuitambua, kuisimamia na kuilinda.
Miongozo hiyo inahusu utambuzi na usimamizi wa miundombinu hiyo, ukaguzi, tathmini ya vihatarishi, uadilifu na uhalisia wa data pamoja na mipango ya kurejesha huduma baada ya kutokea janga.
Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Munaku Mulemwa amesema
hatua hiyo ni muhimu katika kujenga mazingira salama na imara ya kidijitali yatakayowezesha huduma muhimu kuendelea kutolewa kwa ufanisi licha ya kuongezeka kwa changamoto na vitisho vya usalama wa mtandao.
Amesema usajili utaiwezesha Serikali kuwa na uelewa wa miundombinu inayohitaji ulinzi maalumu, kutathmini vihatarishi vinavyoweza kuiathiri na kuweka mazingira bora ya kuilinda dhidi ya vitisho vinavyoendelea kuongezeka.
“Hatua hii inasaidia sana kutambua miundombinu hiyo, kutathmini vihatarishi vinavyoweza kuiathiri na kuweka mazingira bora ya kuilinda dhidi ya vitisho vinavyoendelea kuongezeka katika ulimwengu wa sasa,” amesema Mulemwa.

