Mbunge Kiswaga awafariji watoto wenye mahitaji maalumu – HabariLeo

IRINGA: Zikiwa zimepita mbili tu baada ya kurejea nchini kutoka China alikokuwa katika ziara ya kikazi kwa muda wa wiki tatu, Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Jackson Kiswaga, amekutana na kula chakula pamoja na wanafunzi 145 wenye mahitaji maalumu wanaolelewa na kusoma katika shule ya msingi Kipera iliyopo jimboni mwake.

Kiswaga amesema ameamua kutumia muda huo kuwapa faraja na kuwahakikishia kuwa wanathaminiwa na jamii.

Amesema watoto wenye mahitaji maalumu wana ndoto, matarajio na mahitaji kama watoto wengine, hivyo jamii inapaswa kuwapa upendo, faraja na mazingira yatakayowawezesha kutimiza malengo yao.

“Watoto hawa wana matamanio kama walivyo wanadamu wengine. Mungu aliyewaumba watoto hawa ndiye aliyetuumba sisi sote na anatupenda,” alisema.

Kiswaga alisema uamuzi wa kukaa na kula pamoja na watoto hao ulikuwa zaidi ya kushiriki chakula, bali ni sehemu ya kuwapa ujumbe kwamba hawajatengwa na kwamba Serikali na jamii kwa ujumla zinawajali.

“Nimeona njia pekee ni kukaa nao, tule chakula pamoja na tuzungumze ili wasijione kwamba ni watoto waliotengwa. Serikali inawapenda na mimi kama Mbunge wa Jimbo la Kalenga ninawapenda,” alisema.

Kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Faines Mteleka, wanafunzi 145 wenye mahitaji mbalimbali wanapata elimu na malezi katika shule hiyo.

Alisema wanafunzi hao wana changamoto zinazohusiana na ulemavu wa kuona, kusikia, akili, usonji, ualbino na ulemavu wa viungo.

Mteleka alisema watoto hao wanatoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya Mkoa wa Iringa, na uwepo wa kituo hicho umesaidia kuwawezesha kupata elimu na malezi bila kulazimika kwenda maeneo ya mbali.

“Wanafunzi wanaishi katika mabweni kwa gharama za Serikali. Wanapata chakula cha asubuhi, mchana na jioni, pamoja na huduma za walezi wanaowahudumia mchana na usiku,” alisema.

Alisema Serikali pia imeendelea kuboresha mazingira ya shule hiyo, huku huduma za watoto wenye mahitaji maalumu zikiendelea kuvutia wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali.

Mwalimu huyo alisema shule imepata mafanikio katika kuongezeka kwa uandikishaji wa wanafunzi na ufaulu katika mitihani ya kitaifa.

Hata hivyo, Mteleka alisema bado kuna changamoto ya upungufu wa walimu na vifaa vya kufundishia na kujifunzia vinavyokidhi mahitaji ya wanafunzi wenye changamoto mbalimbali.

“Tuna changamoto ya upungufu wa walimu. Walimu tulionao hawatoshi kuwafundisha wanafunzi wetu ambao ni wengi na wenye mahitaji mbalimbali,” alisema.

Alisema pia bwalo la chakula bado halijakamilika na shule inahitaji msaada wa Serikali na wadau mbalimbali kulikamilisha ili wanafunzi wawe na mazingira bora wakati wa kupata chakula.

Mteleka alisema Serikali pia imeanza ujenzi wa shule ya sekondari katika eneo hilo, ambayo ikikamilika itatoa fursa kwa wanafunzi wenye na wasiokuwa na mahitaji maalumu kuendelea na elimu baada ya kumaliza shule ya msingi.