Wanamichezo kutibiwa bure JKCI – HabariLeo

DAR ES SALAAM: TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imewaalika wanamichezo wote nchini kujitokeza kupima afya bure, huku ikiahidi kutoa matibabu bila malipo kwa wale watakaobainika kuwa na matatizo ya kiafya.

Hatua hiyo inalenga kuimarisha afya za wanamichezo na kuwawezesha kuendelea na shughuli zao za michezo kwa usalama ili kutimiza ndoto zao, hasa katika kipindi hiki cha AFCON.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo, Dk Peter Kisenge, amesema taasisi hiyo imekuwa na utaratibu wa kuwafikishia wananchi huduma za afya na sasa imeelekeza nguvu kwa wanamichezo, na kwamba imejiandaa kikamilifu kuwahudumia wanamichezo kwani ina wataalamu, vifaa vya kutosha na teknolojia za kisasa zinazowezesha uchunguzi wa afya kwa ufanisi.

Kwa mujibu wa Dk Kisenge, amesema Serikali imeiwezesha JKCI kuwa na maabara maalumu na ya kisasa inayotumia teknolojia ya akili bandia (AI), ambayo itasaidia katika utoaji wa huduma mbalimbali za uchunguzi, na vipimo vitakavyotolewa ni pamoja na uchunguzi wa afya ya moyo, kiwango cha sukari, mapigo ya moyo pamoja na vipimo vingine muhimu vya afya.

Aidha, Dk Kisenge amewataka wanamichezo kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara ili kubaini mapema changamoto za kiafya na kupunguza hatari ya vifo vya ghafla wakati wa michezo.

Mchezaji wa pool table, Festo Yohana, ambaye alifika JKCI kwa ajili ya vipimo, ameishukuru taasisi hiyo kwa kuanzisha huduma hiyo bila malipo kwa wanamichezo, kwani wanamichezo wengi hawana utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara, licha ya kushiriki katika shughuli zinazohitaji afya na uimara wa mwili.

Amesema upimaji huo utawasaidia wanamichezo kujua hali zao kiafya, kuchukua hatua mapema endapo watabainika kuwa na changamoto na hivyo kuongeza uwezekano wa kuendelea na michezo yao kwa usalama, na kuwashauri wanamichezo kutumia fursa hiyo kwa kujitokeza kupima afya zao na kuweka afya mbele katika safari yao ya kimichezo.

Kwa upande wake, Balozi wa JKCI, Mrisho Mpoto, amesema lengo la taasisi hiyo ni kuanzisha huduma hiyo ni kupunguza magonjwa ya moyo na magonjwa mengine nchini, huku akisisitiza umuhimu wa kila mtu kufahamu hali yake ya afya.

Amesema ni muhimu zaidi kwa wanamichezo kufahamu viashiria muhimu vya afya zao, ikiwemo kiwango cha sukari, mapigo ya moyo na kiwango cha mafuta mwilini.

Mpoto amesema baadhi ya wanamichezo hufanya mazoezi bila kuzingatia utaratibu unaofaa au bila kufahamu hali ya afya zao, jambo ambalo linaweza kuwaweka katika hatari.

Amesema takwimu zinaonesha kuwa idadi kubwa ya watu hawafahamu hali zao za kiafya, hivyo amewataka wananchi kwa ujumla, pamoja na wanamichezo, kutumia fursa hiyo kwa kufika katika vituo vya JKCI kwa ajili ya vipimo na kupata huduma za matibabu bila malipo.

Hatua hiyo, amesema, inalenga kujenga utamaduni wa uchunguzi wa afya mapema na kusaidia wananchi kuchukua hatua stahiki kabla ya matatizo ya kiafya kuwa makubwa.