
DAR ES SALAAM: Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, ametangaza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali kufuatia maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kumaliza kero za madereva na mgomo uliodumu kwa siku mbili.
Akizungumza leo, Septemba 30, 2026, katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli, Mbezi jijini Dar es Salaam, Katambi amesema maagizo ya Rais yamepitishwa kwa Waziri Mkuu na kuanza kutekelezwa kwa haraka.
Miongoni mwa hatua hizo ni kurejeshwa kwa leseni za madereva, kuondolewa kwa vizuizi visivyo na sababu barabarani pamoja na kushughulikia miundombinu ya barabara, ikiwemo matengenezo ya maeneo yenye mashimo yanayoweza kusababisha ajali.
Kuhusu madereva ambao leseni zao zilikamatwa au kufungiwa kutokana na makosa madogomadogo, Katambi amesema wataweza kurejeshewa leseni zao kwa mujibu wa sheria kupitia Mamlaka ya Rufaa iliyo chini ya Waziri wa Mambo ya Ndani.

Amesema hatua hiyo haitawahusu madereva waliothibitika kuhusika na ajali mbaya zilizosababisha vifo na ambao kesi zao bado zinaendelea mahakamani.
Katambi pia amewataka madereva na wananchi kutafuta suluhisho la changamoto kupitia mazungumzo badala ya migogoro, akisisitiza umuhimu wa Serikali kusikiliza na kuwashirikisha wananchi katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili.
Amesema amepewa mamlaka na Waziri Mkuu kushughulikia malalamiko ya madereva na kwamba changamoto zao sasa zitafanyiwa kazi.
Katika hatua nyingine, Katambi ametangaza kuwa wizara nne za Serikali zitakutana kuchambua na kutafuta suluhisho la changamoto zinazotokana na Mfumo wa Kufuatilia Magari (VTS).
Amesema mkutano huo utazihusisha Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Uchukuzi pamoja na Wizara ya Kazi, Ajira na Mahusiano.
Hatua hiyo imekuja baada ya madereva kulalamikia tofauti za takwimu kati ya mfumo wa VTS na kamera za usalama barabarani.
Kwa mujibu wa Katambi, kuna maeneo ambayo kamera za usalama barabarani zinaweza kuonesha gari lilikuwa likisafiri kwa kasi ya kilomita 100 kwa saa, wakati mfumo wa VTS unaonesha kasi ya kilomita 130 kwa saa.
Amesema tofauti hizo zimekuwa zikisababisha madereva kupata adhabu na kuingia katika changamoto ambazo zinahitaji kufanyiwa tathmini.
Katambi amesema Serikali itakaa pamoja kuchambua changamoto hizo na kuweka utaratibu utakaokuwa na uwazi na haki zaidi kwa madereva.
Aidha, amesema mfumo wa VTS ni wa muda katika kipindi cha mpito, huku Serikali ikielekea kwenye mfumo wa kisasa wa kidijitali wa kudhibiti mwendo wa magari.
Kwa maelezo yake, mfumo huo mpya utakuwa na mfumo wa kamera huru zitakazorekodi makosa ya barabarani moja kwa moja bila kuhitaji udhibiti wa askari.
Katambi amefananisha mfumo huo na VAR inayotumika katika soka, akisema lengo ni kuhakikisha ushahidi wa kamera unatumika katika kuthibitisha makosa na kuongeza usawa katika utekelezaji wa sheria za usalama barabarani.
