SIMANJIRO. Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Qwaray, amewataka waajiri na Mamlaka za Ajira na Nidhamu kuhakikisha changamoto za kiutumishi zinashughulikiwa kwa wakati ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Qwaray ametoa agizo hilo wakati wa kikao kazi cha kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili Watumishi wa Umma katika Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro.
Amesema waajiri wanapaswa kuhakikisha stahiki za watumishi, ikiwemo kupandishwa vyeo, uhamisho, malimbikizo ya mishahara na mafao, zinashughulikiwa kwa wakati kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
Aidha, amesisitiza kuwa madai ya watumishi yanapaswa kuhakikiwa na kuwasilishwa yakiwa yameambatanishwa na nyaraka muhimu ili kurahisisha utatuzi wa changamoto hizo.

Qwaray amezitaka Mamlaka za Ajira na Nidhamu kusimamia haki na wajibu wa watumishi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma, akisisitiza umuhimu wa kuacha utendaji wa mazoea.
Amesema mambo yaliyo ndani ya uwezo wa waajiri na Mamlaka za Ajira na Nidhamu yanapaswa kushughulikiwa katika ngazi hizo badala ya kuendelea kuwasilishwa Ofisi ya Rais.
Kuhusu maadili ya utumishi wa umma, Qwaray amewataka watumishi kuyafahamu na kuyatekeleza kwa kuzingatia Kanuni za Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma.

“Watumishi wanaokiuka maadili au kutotekeleza majukumu yao ipasavyo wanapaswa kuchukuliwa hatua stahiki za kinidhamu kwa wakati,” amesema.
Aidha, amewataka waajiri na Mamlaka za Ajira na Nidhamu kushirikiana na Tume ya Utumishi wa Umma katika ukaguzi wa utekelezaji wa sheria, kanuni na taratibu za kiutumishi na kuhakikisha mapungufu yatakayobainika yanarekebishwa kwa wakati.
