Madereva wa Mabasi Wagoma Nchini, Safari Zasimama

Madereva na wafanyakazi wa mabasi ya masafa marefu wameanza mgomo katika maeneo mbalimbali nchini leo, Septemba 29, 2026, wakipinga faini na adhabu wanazodai kuwa ni kubwa na kuwaweka katika hali ngumu kiuchumi.

Mgomo huo umeathiri shughuli za usafiri katika vituo mbalimbali vya mabasi, ikiwemo Kituo cha Mabasi Magufuli jijini Dar es Salaam, Msamvu mkoani Morogoro na Nane Nane mkoani Dodoma, huku taarifa zikieleza hali kama hiyo kushuhudiwa pia katika Mbeya, Mwanza, Mikumi, Arusha na Kilimanjaro.

Katika Kituo cha Mabasi Msamvu, baadhi ya mabasi yaliyokuwa yamepangwa kuanza safari majira ya saa 12:00 yalionekana kutopakia abiria, huku baadhi ya abiria wakilazimika kurejea nyumbani baada ya safari zao kusitishwa.

Mabasi yaliyoonekana kuendelea kuondoka kituoni ni yale yaliyokuwa yamewasili kutoka safari za masafa marefu na yaliyokuwa yakimalizia safari zao Msamvu.

Madereva hao wanadai kuwa chanzo kikuu cha mgomo ni faini wanazodai kutozwa na askari wa Usalama Barabarani kwa makosa mbalimbali, ambazo kwa baadhi ya makosa zinaweza kufikia hadi shilingi milioni moja kwa dereva.

Mbali na faini, madereva hao wanapinga pia hatua za kusimamishwa leseni, kupunguziwa pointi na hatimaye kupokonywa leseni za udereva.

Wanasema kufungiwa leseni kunawaathiri moja kwa moja kiuchumi kwa sababu wanaposhindwa kuendesha magari hawawezi kufanya kazi wala kupata kipato cha kuendesha maisha yao na familia zao.

Baadhi yao wameeleza kuwa baada ya kurejeshewa leseni, huagizwa kurejea shuleni kwa mafunzo kabla ya kuruhusiwa kuendelea na kazi, jambo ambalo wanasema linaongeza gharama na muda wa kukaa bila kipato.

Katika hali hiyo, baadhi ya madereva waliokutwa katika vituo wamekataa kuzungumza hadharani, huku waliozungumza kwa masharti ya kutorekodiwa wakisema wameamua kusitisha safari kwa kuzingatia pia usalama wao na magari wanayoyaendesha.

Wamedai kuwa baadhi yao waliwaruhusu abiria waliokuwa wamepanga kusafiri kurejea nyumbani kutokana na hofu ya usalama wa magari na watu endapo wangeendelea na safari wakati mgomo ukiendelea.

Madereva hao wamesema wao ndio wenye dhamana ya magari wanayokabidhiwa, pamoja na usalama wa abiria, na hivyo hawataki kuchukua hatua ambayo inaweza kuhatarisha maisha ya watu au mali.

Hatua hiyo inafuatia kauli iliyotolewa Septemba 17, 2026 na madereva wa mabasi ya mikoani na nchi jirani mkoani Mwanza, waliotishia kusitisha huduma kuanzia Septemba 29 kutokana na malalamiko kuhusu kufungiwa leseni zao.

Madereva hao wanataka changamoto wanazozieleza zifanyiwe majadiliano na mamlaka husika, wakisisitiza kuwa wako tayari kushiriki katika vikao vya kutafuta suluhu.

Wakati mgomo ukiendelea, madereva hao wamesema wako tayari kusubiri maelekezo ya viongozi wao na maamuzi yatakayofikiwa katika vikao na mamlaka husika kabla ya kurejea barabarani.

Kwa sasa, kusitishwa kwa safari katika vituo mbalimbali kunaendelea kuleta athari kwa abiria wanaotegemea usafiri wa mabasi kusafiri kwenda mikoa tofauti, huku hali ya usafiri ikiendelea kufuatiliwa.