Polisi Yaonya Wanaochochea Mgomo wa Madereva wa Mabasi – Video

Global Publishers
September 29, 2026
0 views
0 Comments

Jeshi la Polisi nchini limewaonya watu wanaochochea au kushawishi madereva wa mabasi kushiriki katika mgomo, likisisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaokiuka sheria.

Onyo hilo linatolewa wakati baadhi ya madereva wa mabasi yaendayo mikoani wakisimamisha huduma za usafirishaji, wakipinga utekelezaji wa mfumo wa pointi 15 kwenye leseni za udereva.

Mfumo huo unaelekeza kila leseni ya udereva kuanza ikiwa na pointi 15, ambazo hupunguzwa kulingana na makosa ya barabarani anayofanya dereva. Mfumo huo unatokana na kanuni za demerit points zilizowekwa chini ya sheria za usalama barabarani.

Baadhi ya madereva wamekuwa wakipinga utekelezaji wa mfumo huo wakieleza kuwa unaweza kuwa na athari kwa madereva wa kibiashara, hususan kutokana na aina na idadi ya makosa yanayoweza kusababisha kupunguzwa kwa pointi. Mjadala kuhusu mfumo huo umeendelea pia kutoka kwa wadau wanaotaka Serikali kuupitia pamoja na madereva na wadau wengine.

Kwa upande mwingine, mamlaka za usafiri zimeendelea kusisitiza umuhimu wa madereva kuzingatia sheria za barabarani na masharti ya leseni, huku LATRA ikisema inaendelea kusimamia na kuthibitisha madereva wanaohudumu katika sekta ya usafiri wa abiria.

Jeshi la Polisi limewataka wananchi na madereva kuzingatia sheria na kuepuka vitendo vya uchochezi vinavyoweza kuvuruga huduma za usafiri.