NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA MWANZA.
MKUU wa Mkoa wa Mwanza, CP Salum Hamdun, amesema atahakikisha anashirikiana na wananchi wa Wilaya ya Kwimba katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto za maji na barabara zinazowakabili wakazi wa wilaya hiyo.
Amesema utatuzi wa changamoto hizo mbili ni miongoni mwa mambo muhimu yatakayosaidia kuleta tabasamu kwa wananchi wa Kwimba, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, viongozi na wananchi katika kuzitafutia ufumbuzi.
CP Hamduni ameyasema hayo leo Septemba 28, 2026, wakati wa ziara yake ya kujitambulisha kwa watumishi wa Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza, na kueleza kuwa barabara nyingi katika wilaya hiyo zinapitika, lakini bado zinahitaji maboresho ili kuwawezesha wananchi kupata huduma na kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa urahisi zaidi.
Ameeleza kuwa moja ya kilio kikubwa cha wananchi wa Kwimba ni wilaya hiyo kutounganishwa kikamilifu kwa barabara ya lami na makao makuu ya Mkoa.
Aidha ameeleza, kuwa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 hadi Agosti 2026, Wilaya ya Kwimba imepokea zaidi ya Sh bilioni 17 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya barabara.
“Fedha hizo zimetumika katika kuboresha miundombinu ya barabara, hali ambayo imewezesha baadhi ya barabara katika wilaya hiyo kupitika kwa urahisi” Alisema Hamduni.
Aidha amefafanua kuwa katika mwaka wa fedha 2026/2027, wilaya hiyo imetengewa kiasi cha Sh bilioni 4 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya barabara katika maeneo mbalimbali, yakiwemo Kata za Sumve, Ngudu, Hungumalwa, Malya, Mwantale na Mwabomba.
Aidha ameeleza kuwa kwa upande wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), imeelezwa kuwa kuna miradi mbalimbali inayohusisha barabara muhimu katika Wilaya ya Kwimba, ikiwemo kipande cha barabara kutoka Ngudu hadi Mabuki chenye urefu wa kilomita 26, Ngudu hadi Malya kilomita 28, pamoja na barabara ya kiwango cha lami kutoka Hungumalwa hadi Magu yenye urefu wa kilomita 71.
Akisoma taarifa ya Wilaya ya Kwimba mbele ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya hiyo, Ng’wilabuzu Ludigija, alisema changamoto ya maji bado ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili wananchi kutokana na uchakavu wa bomba la maji linalohudumia wilaya hiyo.
Alisema bomba hilo lilianza kutumika tangu mwaka 1975 na kwa sasa limezeeka, hali inayochangia kuwepo kwa changamoto katika upatikanaji wa maji
Hata hivyo, alisema wananchi wanamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuelekeza hatua za kuchukuliwa, ikiwemo kuingia mkataba na mkandarasi kwa ajili ya kubadilisha bomba hilo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ukarabati wa mradi huo utakaogharimu kiasi cha Sh milioni 6 na ukikamilika unatarajiwa kusaidia kuondoa changamoto ya maji inayowakabili wananchi wa Wilaya ya Kwimba.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kwimba, Cosmas Bulala, ameeleza kuwa Wilaya ya Kwimba ndiyo pekee ambayo haijaunganishwa kwa barabara ya lami na makao makuu ya Mkoa wa Mwanza, akieleza umuhimu wa suala hilo kushughulikiwa







