SUA yawajengea uwezo wananchi wanaoshiriki biashara ya kaboni – HabariLeo

MOROGORO: Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kupitia Mradi wa Tathmini ya Mapato ya Kaboni kama Njia Endelevu ya Uwezeshaji Kifedha katika Uhifadhi na Usimamizi wa Misitu ya Jamii Tanzania kimewajengea uwezo maafisa na wananchi kutoka maeneo yenye hifadhi za misitu ya vijiji pamoja na baadhi ya vijiji vyenye misitu ya hifadhi za vijiji ambao wanashiriki biashara ya kaboni na wemeshapata mapato yanayotokana na biashara hiyo.

Wakizungumza wakati wa mafunzo hayo, wananchi wa vijiji ambavyo havijaanza kunufaika na mapato ya kaboni akiwemo Mwanangao Msanya kutoka wilayani Mvomero mkoani Morogoro amesema wamekuwa wakihifadhi misitu ya Kijiji kwa muda sasa lakini mafunzo hayo yamewapa uelewa mpya wa vigezo na taratibu za kuingia na kunufaika na biashara ya kaboni.

Ofisa Misitu Mwandamizi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Siima Bakengesa, akifungua warsha hiyo iliyohusisha wadau kutoka asasi za kiserikali na asasi zisizo za kiserikali na baadhi ya wananchi wa Wilaya za Tanganyika, Mbulu, Mvomero, Mwanga na Korogwe, amesema mafunzo hayo ni muhimu katika kuimarisha uhifadhi wa bioanuwai na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia usimamizi shirikishi wa misitu ya vijiji.

Mtafiti Kiongozi wa Mradi, Dk. Kajenje Nkukurah amesema SUA inaamini mafunzo hayo yatawezesha vijiji ambavyo bado havijaingia katika biashara ya kaboni kufanya maamuzi sahihi kuhusu ushiriki wao pamoja na kuimarisha utawala na usimamizi wa mapato katika ngazi ya vijiji.

Aidha amesema mradi unalenga kuwajengea uwezo wananchi wa vijiji vyenye misitu iliyo katika biashara ya kaboni ili waweze kuendelea kunufaika kiuchumi kupitia biashara ya kaboni, huku mapato yakitumika katika usimamizi endelevu wa misitu ya hifadhi ya vijiji na kuchochea maendeleo endelevu.

Akitoa ushuhuda wakati wa kuwasilisha sauti za jamii, Ofisa Misitu wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Bruno Mwaisaka amesema wilaya hiyo imepokea zaidi ya shilingi bilioni 34 kutokana na biashara ya kaboni ambapo fedha hizo zimechangia kuboresha ustawi wa jamii kupitia ujenzi wa shule, vituo vya afya na kutoa ajira za muda kwa wananchi huku pia zikiongeza ari ya jamii kushiriki katika uhifadhi na usimamizi wa misitu.

Mradi wa Tathmini ya Mapato ya Kaboni kama Njia Endelevu ya Uwezeshaji Kifedha katika Uhifadhi na Usimamizi wa Misitu ya Jamii Tanzania ni wa miaka mitatu unaotekelezwa na SUA kama taasisi inayoongoza, kwa kushirikiana na NCMC na Chuo Kikuu cha Bangor cha Uingereza ukifadhiliwa na Defra kupitia GCBC, DAI, ISPF pamoja na Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Serikali ya Uingereza.