Serikali yatambua mchango wa Saccos ustawi wa watu – HabariLeo

MOROGORO: SERIKALI imesema inatambua kuwa vyama vya ushirika na saccos nchini vina mchango mkubwa katika kukuza uchumi kwa wananchi na kwa kupitia Saccos  wanaweza kuweka akiba, kupata mikopo kwa masharti nafuu , kukuza biashara na kuimarisha ustawi wa familia.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhandisi Mshamu  Munde, amesema hayo akifungua mkutano mkuu wa 13 wa mwaka wa wawakilishi wa Hazina Saccos Ltd mjini Morogoro .

Mkutano mkuu huo ulilenga kujadili taarifa mbalimbali na kupitia hali ya kifedha , kutathimini utekelezaji wa maamuzi ya mkutano mkuu uliopita, kuweka vipaumbele kwa kipindi kijacho na kufanyika uchaguzi wa viongozi wapya.

Naibu Waziri amesema Serikali kupitia Wizara hiyo inaziagiza  Saccos ikiwemo ya  Hazina iendelee kuwa mfano wa chama kinachotoa huduma  bora , kuendesha shughuli zake kwa kuzingatia sheria, kanuni , miongozo ya serikali na kutuza  fedha za wanachama.

Amesema kupitia Saccos zao wananchi wanaweza kukusanya nguvu zao za kiuchumi na kupata huduma ambazo wakati mwingine ni vigumu kuzipata wakiwa mmoja mmoja .

“ Kuna umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa Saccos ili ziongeze weledi , uwazi na uwajibikaji,” amesisitiza Mhandisi  Munde.

Mhandisi Munde amesema mikopo inatotolewa na Hazina Saccos  imewawezesha wanachama wake kuendesha biashara , kujenga nyumba , kugharamia elimu , kukabiliana na dhoruba na kutekeleza shughuli za maendeleo.

Ameipongeza Hazina Saccos kwa utoaji wa mikopo kwa wanachama ambapo  wanawake  wameendelea kuwa kundi kubwa la wakopaji wakiwa ni asilimia 55.4 .

“ Jambo hili ni kubwa na  kama inavyofahamika  hata iliyokuwa kwenye asilimia 10  na sasa asilimia 15 ya mapato ya ndani ya Halmashauri , wakopaji na walipaji wazuri ni wanawake” amesema Mhandisi Munde.

Amesema kuwa inaonesha Hazina Saccos ina nachangia kuwezesha wanawake kiuchumi na kutekeleza azma ya serikali ya kuongeza ujumuishi kwa kifedha.

Mhandisi Munde  ameitaka Menejimenti ya Hazina Saccos kuhakikisha kuwa fedha za wanachama zinalindwa kwa kiwango cha juu ambalo ni matumaini makubwa ya wanachama.

Amewataka wanachama kutumiza wajibu wao kwa kuweka akiba kwa utaratibu na kurejesha mikopo kwa wakati kwani Saccos haiwezi kukua ikiwa hawataweka akiba na kutimiza masharti ya mikopo.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Hazina SACCOS Limited,Dk  Festo Mwaipaja  amesema katika  kipindi cha Januari hadi Agosti 2016  wanachama imeongezeka  kwa kasi kwa kufikia 12,000  kutoka 10, 326 waliokuwepo mwishoni mwa mwaka 2025.

Amesema Hazina Saccos imefanikiwa kuongeza mali  zake kutoka takribani bilioni 49.4 mwaka 2025  kufikia  takribani Sh bilioni 63.75  mwezi Agosti mwaka huu (2026), na amana za wanachama zimeongezekakufikia bilioni 50 wakati bakaa ya mikopo imefikia  takribani sh bilioni 48.5 .

Dk Mwaipaja amesema kwa kipindi cha miezi minane cha mwaka huu mikopo  2,318 yenye thamani takribani Sh bilioni 22.8 ilitolewa na  wanawake waliongoza kuchukua mikopo ikiwa ni asilimia 55.4.