Jazzma Kendrick Afichua Sababu ya Kuachana na Rick Ross

Global Publishers
September 28, 2026
0 views
0 Comments

Siku chache tangu mwanamitindo mashuhuri nchini Marekani, Jazzma Kendrick atangaze rasmi kuvunja uhusiano wake wa kimapenzi na rapa mkongwe Rick Ross, mapya yameibuka baada ya mrembo huyo kudai kuwa aliachana na rapa huyo kwa sababu alikuwa akimfanyia ukatili wa kimwili ikiwemo kumpiga.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, Jazzma ameeleza kuwa alipigwa ngumi ya mdomo na msanii huyo, tukio lililomfanya afikie uamuzi wa kuondoka kwenye uhusiano huo.

Mwanamitindo huyo aliongeza kuwa shambulio hilo limemdhihirishia wazi kwamba Rick Ross hana upendo wa dhati kwake.

Tukio hilo limevuta hisia za watu wengi, ikiwa ni pamoja na rapa 50 Cent ambaye ameingilia kati suala hilo kwa kumsemea mbovu hasimu wake huyo wa muda mrefu.

Akizungumzia mkasa huo, 50 Cent alidai kuwa kitendo alichofanya Rick Ross kinatokana na msongo wa mawazo unaomkabili, baada ya albamu yake mpya ya ‘Set In Stone’ kubuma.

Uhusiano wa Jazzma Kendrick na Rick Ross ulianza kuwekwa wazi katikati ya mwaka 2025, ambapo wawili hao walianza kuonekana pamoja hadharani na kupost picha na video za kimapenzi kwenye mitandao ya kijamii.

Hata hivyo, uhusiano wao umekuwa wa kuingia na kutoka (on-and-off relationship), ukikumbwa na migogoro pamoja na kutengana kwa muda mfupi mara kadhaa kabla ya kuibuka kwa tuhuma hizi za hivi karibuni za shambulio la kimwili lililosababisha Jazzma kutangaza kuondoka jumla.

Hadi sasa, Rick Ross hajatoa tamko lolote au kujibu tuhuma hizo za shambulio zilizoelekezwa kwake.

Stori na Hasina Thabit | GPL