ARUSHA: KUIMARISHA tafiti za kitaaluma na kutumia matokeo yake kutatua changamoto zinazoikabili jamii ni miongoni mwa malengo ya Taasisi ya Usimamizi ya Afrika Mashariki na Kusini (ESAMI).
Uimarishaji wa tafiti hizo umeelezwa kupitia programu mpya za shahada za uzamivu katika Usimamizi wa Biashara (DBA) na Uzamivu wa Falsafa (PhD).
Mkurugenzi Mkuu wa ESAMI, Profesa Peter Kiruku, alisema hayo wakati wa uzinduzi rasmi wa programu hizo, akieleza kuwa utafiti wa kitaaluma unapaswa kwenda zaidi ya kuongeza maarifa na kulenga kuboresha maisha ya watu.

Alisema Afrika na dunia kwa ujumla zinahitaji maarifa mapya na ujuzi wa kiwango cha juu kutokana na mabadiliko yanayoendelea katika taasisi, mashirika na sekta mbalimbali.
Kwa mujibu wa Profesa Kiruku, tafiti zinapaswa kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika mazingira yao na kutoa matokeo yenye tija kwa jamii.
Alisema uzinduzi wa programu hizo ni sehemu ya hatua za ESAMI kukabiliana na mahitaji yanayobadilika ya elimu ya juu na uongozi barani Afrika.
Naye, Mkurugenzi wa Biashara wa ESAMI, Profesa Joseph Mumba, alisema programu hizo zote ni shahada za uzamivu zinazohusisha utafiti, lakini zinatofautiana katika msisitizo wa tafiti zake.
Alisema shahada ya PhD inalenga zaidi utafiti wa kinadharia na kuzalisha maarifa mapya katika maeneo ya kitaaluma, wakati DBA inalenga kutumia utafiti kutatua changamoto halisi za biashara na taasisi.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Global Humanistic University, Profesa Mario Grabner, alisema ushirikiano huo unalenga kuwezesha watu kupata elimu ya juu bila kulazimika kuacha familia na maeneo yao ya kazi.
Alisema mtandao wa kitaaluma wa taasisi hiyo unajumuisha washauri na maprofesa zaidi ya 150 kutoka nchi zaidi ya 37, huku programu hizo zikiwa na mtazamo wa kimataifa unaozingatia mahitaji ya Afrika.
Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa ESAMI, Profesa David Kalaba alisema taasisi hiyo inalenga kutumia uzoefu wake wa kikanda na ushirikiano wa kimataifa kuongeza fursa za elimu ya uzamivu kwa wataalamu.
Alisema programu hizo zinaweza kuwawezesha wataalamu kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki na Kusini kuendelea na masomo bila kulazimika kuhama maeneo yao ya kazi.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi, watumishi wa ESAMI, wahitimu, wasomi na wanafunzi watarajiwa wa programu hizo.
