Global Publishers
September 27, 2026
12 views
0 Comments

Watalii waliokuwa katika safari ya kujionea wanyamapori nchini Namibia wamekumbwa na hofu baada ya kifaru mweusi kulishambulia gari lao katika Hifadhi ya Taifa ya Etosha.
Tukio hilo lilirekodiwa na Ebot Enow Ebot Agbor Ndip, ambaye ni mwongoza watalii, na video hiyo baadaye kushirikishwa na Storyful.
Katika video hiyo, kifaru huyo anaonekana akilikimbilia gari lililokuwa barabarani, kabla ya kuligonga kwa nguvu kwa kichwa na pembe zake upande wa kushoto wa gari.
Nguvu ya mashambulizi hayo ilisababisha sehemu ya gari kung’oka, huku kifaru huyo akiendelea kulisukuma na kuligonga. Magari mengine yaliyokuwa nyuma yalisimama baada ya kuona tukio hilo.
Baadaye, dereva wa gari lililokuwa likishambuliwa alianza kuliondoa eneo hilo, huku kifaru huyo akilifuatilia kwa muda kabla ya kusimama.

Kwa mujibu wa taarifa za tukio hilo, watalii waliokuwa ndani ya gari walifanikiwa kuondoka salama bila kupata majeraha, ingawa gari lilipata uharibifu.
Ndip alisema kifaru huyo alionekana kuwa katika hali ya kuchanganyikiwa na kwamba alijitahidi kuweka umbali salama wakati akirekodi tukio hilo.
Hata hivyo, alieleza kuwa baadhi ya magari mengine hayakuweka umbali huo, na akaonya kuwa watalii wanaoendesha magari wenyewe katika hifadhi wanapaswa kufahamu tabia na ishara za wanyama kabla ya kuwakaribia.
Msemaji wa Wizara ya Mazingira, Misitu na Utalii ya Namibia, Vilho Hangula, aliwahimiza watalii kuwa waangalifu wanapokuwa katika hifadhi za wanyamapori.
Hangula alisema wanyama wa porini huongozwa na tabia zao zinaweza kuwa zisizotabirika.
Mamlaka pia zimewashauri watalii kutumia waongozaji wenye uzoefu na walioandikishwa, pamoja na kujifunza tabia za wanyama wa porini ili kupunguza hatari wakati wa safari.
