Leo ni siku ya Utalii Duniani ambapo Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro inaungana na wadau wengine duniani kusherehekea sikukuu hii ikiwa imejipanga kuendeela kuhudumia watalii kwa viwango vya kimataifa na kuendelea kuwahimiza wapendanao kuja kushuhudia maajabu ya dunia katika bustani ya Eden.
Kutokana na upekee wa Ngorongoro ambapo hadithi, fikra na mtazamo wako unakutana na uhalisia ukija bila mpenzi wako utapata tabu ya kumsimulia mwenzako kutokana na utakayoyaona kwani ni hifadhi iliyojaa kila aina ya vivutio ambavyo si fahari ya Tanzania pekee bali dunia nzima
Akizungumzia kuhusu maajabu ya Ngorongoro kamishna Msaidizi Mwandamizi anayesimamia huduma za utalii na Masoko Mariam Kobelo amesema kwamba Hifadhi ya Ngorongoro ni urithi uliotukuka ambao unahitaji kulindwa kwa wivu mkubwa kwa maslahi ya vizazi vijavyo.
Kobelo anaeleza kuwa katika kuadhimisha Siku ya Utalii Duniani 2026, Mamlaka inawashukuru kwa dhati wageni waendeshaji wa utalii, mawakala wa safari, washirika ,wawekezaji, waongoza watalii, wadau wa sekta ya utalii na jamii kwa mchango mkubwa katika utalii.
“Tunapoelekea katika mustakabali mpya wa utalii, Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro inaendelea kufanya maboresho mbalimbali katika huduma za kidijitali na matumizi ya Akili Unde (Artificial Intelligence – AI) ili kuongeza ufanisi, kuboresha uzoefu wa wageni na kutoa huduma zinazokidhi viwango vya kimataifa, huku tukizingatia msingi wetu mkuu wa uhifadhi na utalii endelevu” amesisitiza kamishna Kobelo
Ameongeza kuwa Ngorongoro si eneo la kutembelea tu bali ni urithi wa dunia unaopaswa kuishi kwa faida ya vizazi na vizazi kuendelea kujifunza kutokana na historia ya asili iliyofunikwa na tabasamu la uhifadhi endelevu. Ngorongoro inathamini utamaduni wetu, tunahifadhi maliasili zote kwa kutambua kuwa maendeleo ya utalii yanaenda sambamba na wajibu wa kulinda mazingira na kuhifadhi urithi wetu kwa ajili ya vizazi vijavyo
‘Katika siku hii muhimu, ninawaalika wote kuendelea kuwa sehemu ya safari hii, Tuitembelee Ngorongoro, Tuiheshimu Ngorongoro, Tuilinde Ngorongoro, Tuiache Ngorongoro ikiwa bora kwa vizazi vya sasa na vijavyo na kuhakikisha tunaenda sambamba na kauli mbiu yam waka huu isemayo “Ajenda ya Kidijitali na Akili Bandia Kubuni Upya Sekta ya Utalii,”
Heri ya Siku ya Utalii Duniani 2026.
