China Yaitaka Marekani Kuheshimu Nchi za Ghuba na Kuondoa Vikwazo Cuba

NEW YORK: China imetumia hotuba yake katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa kupinga baadhi ya sera za Marekani kuhusu Iran na Cuba, ikisisitiza kuheshimiwa kwa mamlaka na usalama wa nchi za Ghuba na kutaka kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya Cuba.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa 81 wa Umoja wa Mataifa Jumamosi, Septemba 26, 2026, Makamu wa Rais wa China, Han Zheng, hakuitaja Marekani moja kwa moja, lakini alitoa wito kwa nchi zenye nguvu kuheshimu sheria za kimataifa na kutotumia vitisho vya nguvu dhidi ya mataifa mengine.

“China inaamini kwamba mamlaka na usalama wa nchi za Mashariki ya Kati, ikiwemo nchi za Ghuba, vinapaswa kuheshimiwa,” Han alisema.

Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kukutana na Rais wa China, Xi Jinping, katika mazungumzo yaliyofanyika White House.

China yazungumzia Iran

Han pia alisisitiza kwamba nchi kubwa zina wajibu maalumu katika kulinda amani na usalama wa kimataifa na zinapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuheshimu sheria za kimataifa.

Msimamo huo unakuja wakati mzozo kati ya Marekani, Israel na Iran ukiendelea, huku Washington ikiendelea kuweka shinikizo dhidi ya Tehran.

Balozi wa Marekani nchini China amesema Trump alimuonya Xi kuhusu kutoa msaada kwa Iran wakati wa mazungumzo yao, huku akisema China ilitoa hakikisho kwamba haitafanya hivyo.

Ripoti pia zimeibua madai kwamba Beijing imeisaidia Tehran kukabiliana na vikwazo, ikiwemo katika masuala ya mauzo ya mafuta na vifaa vya ulinzi. Madai hayo yamekuwa sehemu ya mvutano mpana wa kisiasa kati ya Washington na Beijing.

China yataka vikwazo dhidi ya Cuba viondolewe

Katika hotuba hiyo, Han pia aliitaka Marekani kusitisha kile alichokiita vitisho vya kutumia nguvu dhidi ya Cuba na kuondoa vikwazo na zuio la kiuchumi dhidi ya nchi hiyo.

“China inatoa wito kwa nchi husika kusitisha mara moja matumizi ya vitisho vya nguvu dhidi ya Cuba na kuondoa kikamilifu zuio na vikwazo dhidi yake,” Han alisema.

Kauli hiyo imekuja wakati Cuba ikikabiliwa na changamoto kubwa za nishati na miundombinu, huku kukiwa na matatizo ya upatikanaji wa mafuta na kukatika kwa umeme.

Baadaye, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergey Lavrov, pia alitoa wito wa kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya Cuba. Lavrov alitaka Washington kuondoa kile alichokiita “kuzingirwa” kwa Cuba na pia kuondoa vikwazo vya biashara.

Han alitumia hotuba yake pia kusisitiza nafasi ya China kama mshirika wa nchi zinazoendelea, akisema mataifa yote, makubwa na madogo, yanapaswa kuwa na usawa katika jumuiya ya kimataifa.

Alisema masuala ya dunia yanapaswa kushughulikiwa kupitia mashauriano ya pamoja badala ya maamuzi ya upande mmoja.