Waandaaji Tamasha la Miaka 30 ya Bongo Fleva Walipa Faini ya Dudu Baya

Global Publishers
September 26, 2026
12 views
0 Comments

Waandaaji wa Tamasha la Miaka 30 ya Bongo Fleva wametangaza kutekeleza adhabu iliyotolewa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), ikiwemo kumlipia msanii Godfrey Tumaini, maarufu kama Dudu Baya, faini ya Sh milioni tatu.

Kupitia taarifa iliyotolewa leo na mmoja wa waratibu wa tamasha hilo, Madee Ali, amesema baada ya kupokea maamuzi ya BASATA, wamekubali kuyatekeleza na kwa haraka wamelipa faini iliyotolewa kwa waandaaji, pamoja na faini iliyotolewa kwa Dudu Baya.

Waandaaji hao wameihakikishia BASATA pamoja na wadau wa sanaa nchini kuwa wanaheshimu maamuzi yaliyotolewa na wataendelea kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia taratibu, kanuni na sheria zilizowekwa.

Aidha, wamesema ushirikiano, uwajibikaji na uzingatiaji wa sheria ni miongoni mwa misingi muhimu katika kulinda, kukuza na kuendeleza sekta ya sanaa nchini.

“Tunatoa shukrani kwa BASATA na wadau wote kwa ushirikiano wao, huku tukiahidi kuendelea kushirikiana na mamlaka husika katika kuhakikisha sekta ya sanaa inakua na kuendelezwa kwa kuzingatia misingi ya kisheria na kitaaluma,” amesema Madee.