Babu adai kupigwa ngwara na mwalimu Bahi
Bahi. Mvutano kati ya mzee mwenye umri wa miaka 86, anayemtuhumu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mpamantwa kwa madai ya kumpiga ngwara, umeingia sura mpya baada ya Serikali ya Kijiji kueleza ilivyopokea na kushughulikia malalamiko hayo.
Tukio hilo linamhusisha mzee Joseph Ndega, maarufu Shamba, anayedai mwalimu mkuu wa shule hiyo, Ramadhan Kipenya, kumpiga ngwara Agosti 4, 2026, baada ya kufika shuleni hapo kuulizia adhabu walizopewa wajukuu zake pamoja na wanafunzi wengine.
Kwa mujibu wa Shamba, aliamua kwenda shuleni baada ya wajukuu zake kurudi nyumbani wakilalamika kupigwa viboko vingi.
Amesema alipofika na kumsogelea mwalimu mkuu, alikasirika na kumshambulia.
“Watoto walirudi wanalia, wakasema wamepigwa sana, nikaamua kwenda kuwasikiliza na kujua chanzo. Lakini, aliponiona akapatwa na hasira. Baada ya kumsogelea akanipiga ngwara, tukaanguka wote, ndipo akanipiga makofi mawili,” amesema.
Shamba anasema hakufikisha malalamiko yake kwa viongozi wa ngazi za juu kwa sababu alielekezwa kuwa suala hilo lilipaswa kumalizwa katika ngazi ya kijiji.
Ameongeza kuwa anaamini tabia ya kupiga wanafunzi imekuwa ikijitokeza shuleni hapo, na ndiyo iliyomsukuma kufuatilia suala hilo baada ya wajukuu wake kupewa adhabu.
Akijibu tuhuma hizo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mpamantwa, Ally Kipenya, amekana kumpiga Mzee Shamba.
“Kwa sasa niko benki, kwa hiyo siwezi kulisema sana jambo hili, ila kifupi halipo na sijawahi kufanya hivyo. Labda watu wangesikia huko, nikitoka nitakutafuta,” amesema.
Hata hivyo, baada ya mazungumzo hayo, Kipenya hakupatikana tena kwa simu.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mpamantwa, John Makolokolo, amekiri kuwepo kwa mvutano huo, lakini amekanusha madai kuwa mwalimu mkuu alimpiga mzee Shamba.
Amesema baada ya mzee Shamba kufika kijijini kulalamikia adhabu za wajukuu wake, Serikali ya Kijiji ilimuita mwalimu mkuu kwa mahojiano.
“Mwalimu mkuu alituambia siku hiyo alimkuta mzee Shamba anavutana na mwalimu wa zamu, ndipo akamshika mkono na kumtoa eneo hilo ili kuzuia mvutano. Hapo ndipo hali ilipotulia,” amesema Makolokolo.
Kuhusu madai ya wanafunzi kuchapwa viboko vingi, Makolokolo amesema si kweli kuwa walimu wana utaratibu huo, akisema adhabu zinazotolewa ni za kawaida.
Amesema siku hiyo wajukuu wa Shamba waliitwa na Serikali ya Kijiji ilimtuma mtendaji pamoja na ofisa maendeleo wa kijiji, ambao waliwakagua na kutoa taarifa kuwa hawakuona alama zilizoashiria walipigwa viboko kupita kiasi.
Makolokolo amesema Shamba amekuwa akihusika katika migogoro kadhaa katika maeneo tofauti, hasa anaposikia wajukuu wake wamepewa adhabu.

