Marekani Yakataa Viza ya Mkuu wa Jeshi la Sudan Mkutano wa UN

Global Publishers
September 25, 2026
0 views
0 Comments

Marekani imezuia viza ya mkuu wa jeshi la Sudan, Abdel Fattah al-Burhan, kabla ya safari yake iliyopangwa kwenda New York kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), hatua inayoongeza mvutano kati ya Washington na jeshi la Sudan.

Kwa mujibu wa Reuters, chanzo cha ngazi ya juu nchini Sudan kimesema Burhan ameahirisha safari yake kwenda New York, ingawa bado hajapokea taarifa rasmi kuhusu kukataliwa kwa viza. Serikali ya Sudan imeelezea hatua hiyo kama ukiukaji wa Mkataba wa UN na sheria za kimataifa, ikisisitiza kuwa iko tayari kwa amani.

Balozi wa Sudan katika UN amemwomba Katibu Mkuu wa Umoja huo, Antonio Guterres, kuingilia kati suala hilo. Katika barua yake, balozi huyo amesema kumzuia Burhan kuhudhuria Mkutano Mkuu wa UN kunakiuka wajibu wa Umoja huo kwa nchi wanachama.

Chanzo cha kidiplomasia cha Sudan kimeiambia Reuters kuwa maafisa wa Marekani wameweka sharti kwamba Burhan akubali kusitisha mapigano kwa siku 90 ili kuhudhuria mkutano huo.

Pendekezo hilo linahusishwa na Mshauri Mkuu wa Marekani anayehusika na Masuala ya Waarabu na Afrika, Massad Boulos. Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani haikutoa maoni kuhusu viza hiyo.

Marekani imesema Jeshi la Sudan (SAF), kikosi cha Rapid Support Forces (RSF) na viongozi wao “hawawakilishi utawala halali wa kikatiba nchini Sudan.” Burhan alitarajiwa kuhutubia Mkutano Mkuu wa UN leo, lakini hotuba hiyo itatolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan, Mohieldin Salem hatua hiyo inatokea wakati vita vya Sudan vilivyoanza Aprili 2023 vikiendelea.