OSHA, Bulyanhulu wapongezwa usalama kazini – HabariLeo

SHINYANGA: KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeipongeza Ofisi ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) pamoja na Mgodi wa Bulyanhulu kwa kuwekeza katika mifumo ya usalama na afya ya wafanyakazi, hatua inayolenga kuwalinda dhidi ya vihatarishi vinavyoweza kujitokeza katika mazingira ya kazi.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Hawa Chakoma, wakati wa ziara ya kamati katika Mgodi wa Bulyanhulu mkoani Shinyanga, iliyolenga kufuatilia utekelezaji wa Sheria Na. 297 ya mwaka 2023 kuhusu Usalama na Afya Mahali pa Kazi, inayosimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano.

Chakoma amesema ziara hiyo imelenga kutathmini namna wafanyakazi wanavyolindwa dhidi ya vihatarishi vinavyotokana na shughuli za uchimbaji wa madini, pamoja na ufanisi wa mifumo iliyowekwa kuwasaidia wafanyakazi wanaopata ajali au changamoto za kiafya wakiwa kazini.

“Tunataka kuona ni kwa namna gani wenzetu wa mgodi wanajaribu kuondoa vihatarishi kwa wafanyakazi, au kuwahudumia wanaopata changamoto hizo wakiwa mahali pa kazi,” amesema Chakoma.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Dkt. Evaline Wilbard Munisi, amesema Serikali kupitia OSHA imeendelea kuimarisha usimamizi wa usalama na afya mahali pa kazi kwa kufanya kaguzi, kutoa elimu na kuhakikisha waajiri wanazingatia matakwa ya sheria.

Dk Munisi amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026, jumla ya kaguzi 871 zilifanyika mkoani Shinyanga, huku wafanyakazi 7,969 wakifanyiwa vipimo vya afya.

Amesema pia jumla ya waajiri 102 walikidhi matakwa ya sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi na kupatiwa vyeti vya ithibati, wakati waajiri wengine walipewa maelekezo ya kufanya maboresho katika maeneo yaliyobainika kuwa na changamoto.

Katika upande wa mafunzo, Dkt. Munisi amesema jumla ya wafanyakazi 931 walipatiwa mafunzo kuhusu usalama na afya mahali pa kazi katika kipindi hicho.

Amesisitiza kuwa hatua hizo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha maeneo ya kazi yana mifumo madhubuti ya kuzuia ajali, magonjwa yatokanayo na kazi na madhara mengine yanayoweza kuhatarisha afya na usalama wa wafanyakazi.

Naye Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema taasisi hiyo inaendelea kusimamia usalama na afya mahali pa kazi kwa kuhakikisha waajiri wanaweka mifumo madhubuti ya kuwalinda wafanyakazi dhidi ya vihatarishi.

Amesema OSHA pia inaweka mkazo katika utoaji wa elimu na uhamasishaji ili waajiri waelewe wajibu wao kisheria na waweze kutekeleza matakwa ya usalama na afya mahali pa kazi kwa ufanisi.

Ziara hiyo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake ya kufuatilia utekelezaji wa sheria pamoja na maagizo na maelekezo yaliyowahi kutolewa kuhusu uboreshaji wa usalama na afya mahali pa kazi.