
DAR ES SALAAM, Septemba 24, 2026 — Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, ameendelea kutoa majumuisho yake ya mwisho katika kesi ya uhaini inayomkabili, akisisitiza kuwa Mahakama inapaswa kutathmini kama maneno anayodaiwa kuyasema yanaweza, kwa mujibu wa sheria, kuunda kosa la jinai linalomkabili.
Lissu ametoa hoja hizo mbele ya jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu, akiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, katika hatua ya mwisho ya kesi hiyo. Anashtakiwa kwa kosa la uhaini chini ya kifungu cha 39(2)(d) cha Kanuni ya Adhabu, kuhusiana na madai ya kuchochea umma kuzuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Katika majumuisho yake, Lissu amesema hoja yake siyo tu kuhusu iwapo alitamka maneno yanayodaiwa na upande wa mashtaka, bali kama maneno hayo, yakitazamwa pamoja na mazingira yaliyotolewa, yanatimiza vipengele vinavyotakiwa kisheria kuthibitisha kosa la uhaini.
Amesema maneno yanayodaiwa kutamkwa katika mkutano wa Aprili 3, 2025, yakiwemo madai ya “tutazuia uchaguzi”, “tutahamasisha uasi” na “tutakinukisha vibaya”, hayajafafanuliwa na upande wa mashtaka kuhusu namna yanavyounda kosa la jinai.
Kwa mujibu wa Lissu, si wajibu wa mshtakiwa kufafanua kwa niaba ya upande wa mashtaka maana ya maneno hayo au kueleza kwa nini hayakuwa kosa. Amesema jukumu hilo liko kwa upande wa mashtaka kuonyesha kwa ushahidi kwamba maneno hayo yanatimiza masharti ya kosa analoshtakiwa.
Lissu pia amejikita katika hoja ya madai kwamba maneno yake yalilenga kuitishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amehoji ni chombo gani au kiongozi gani wa Serikali anayedaiwa kutishiwa, akitaja kwa mfano Rais, Makamu wa Rais, Serikali yenyewe au taasisi nyingine.
Hoja hiyo inaendana na hoja aliyoiwasilisha katika siku ya kwanza ya majumuisho, ambapo alisema hati ya mashtaka haijaeleza kwa usahihi ni sehemu gani ya Serikali iliyodaiwa kutishiwa.
Lissu pia amesema katika maneno yanayodaiwa kutamkwa hakuna mahali ambapo ametaja Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais, Makamu wa Rais au kiongozi mwingine wa Serikali.
Kwa upande wake, upande wa mashtaka unasema mazingira na maudhui ya kauli hizo yanaonyesha dhamira ya kutishia Serikali na kuzuia uchaguzi.
Katika kuchambua ushahidi, Lissu amesema ushahidi wa baadhi ya mashahidi wa Jamhuri unatofautiana kuhusu maana ya maneno aliyodaiwa kuyasema.
Ametaja PW1, PW2 na PW16 kama mashahidi waliotoa tafsiri kwamba kauli hizo zilihusisha tishio kwa Serikali, huku akisema PW17, ambaye alikuwa katika mkutano huo, hakutoa tafsiri hiyo.
Kwa mujibu wa Lissu, PW17 alikuwepo kwenye mkutano wa Aprili 3, 2025 na alisikiliza yaliyokuwa yakijadiliwa, ikiwemo sera ya CHADEMA ya “No Reform, No Election.”
Lissu amesema ushahidi wa PW17 unaunga mkono hoja ya utetezi kwamba mkutano huo ulihusisha mjadala kuhusu sera ya chama na changamoto za mfumo wa uchaguzi.
“Kesi imejengwa kwenye hisia”
Lissu amesema anachopinga ni tafsiri ya upande wa mashtaka kwamba kauli hizo zilikuwa na nia ya kuitishia Serikali.
Amedai kuwa msingi huo unatokana na hisia au tafsiri ya mashahidi badala ya ushahidi unaoonyesha moja kwa moja nia hiyo.
Amesema ushahidi wa upande wa utetezi unaonyesha kuwa lengo lake lilikuwa kueleza msimamo wa CHADEMA kuhusu mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi na sera ya “No Reform, No Election”, na kwamba hakulenga kuitishia Serikali wala kuhamasisha vurugu.
Katika hatua hiyo, Lissu pia amesisitiza kuwa Mahakama inapaswa kuzingatia ushahidi uliotolewa na pande zote kabla ya kufikia hitimisho kuhusu nia yake.
Arejea kesi ya Freeman Mbowe
Lissu amerejea pia uamuzi wa Mahakama katika kesi iliyomhusu aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, akisema uamuzi huo una umuhimu katika hoja yake kuhusu ulazima wa hati ya mashtaka kueleza kwa uwazi tuhuma zinazomkabili mshtakiwa.
Amesema sheria inapaswa kumpa mtu anayeshtakiwa taarifa ya kutosha kuhusu kosa analodaiwa kutenda ili aweze kuandaa utetezi wake.
The Chanzo imeripoti kuwa Lissu alitumia pia uamuzi wa Isdory Patrice kuunga mkono hoja kwamba mshtakiwa anapaswa kupewa maelezo ya kutosha ya tuhuma ili aweze kujitetea ipasavyo.
Kesi iko hatua ya mwisho
Upande wa Jamhuri ulifunga ushahidi wake Agosti 17, 2026 baada ya kuwaita mashahidi 17 kati ya 30 waliokuwa wameorodheshwa. Mahakama baadaye iliamua kuwa Lissu ana kesi ya kujibu, na upande wa utetezi ukafunga ushahidi wake Septemba 18.
Kwa sasa, pande zote zinaendelea na majumuisho ya mwisho kabla ya jopo la majaji kufanya tathmini ya hoja na ushahidi uliowasilishwa.
Lissu amesema uamuzi wa kesi hiyo hautamhusu yeye pekee, bali unaweza pia kuweka msingi wa kisheria utakaozingatiwa katika kesi zijazo.
Stori na mwandishi Wetu
