Global Publishers
September 24, 2026
0 views
0 Comments

Jaji wa Mahakama ya Shirikisho nchini Marekani, Timothy Kelly, ameamuru utawala wa Rais Donald Trump kurejesha mara moja vibali vya waandishi wa habari kutoka CNN, MS NOW na Politico vya kuingia na kufanya kazi katika Ikulu ya Marekani, White House.
Uamuzi huo umetolewa baada ya vyombo hivyo kufungua kesi kupinga hatua ya utawala wa Trump kuviondoa katika shughuli za White House.
Jaji Kelly ametoa amri ya muda ya siku 14, huku akisema marufuku hiyo inaonekana kuwa na matatizo ya kikatiba na kwamba waandishi hawakupewa utaratibu unaostahili kabla ya vibali vyao kufutwa.
Tukio hilo lilianza baada ya Trump kutangaza Septemba 18, 2026 kuwa CNN, MS NOW na Politico havitaruhusiwa tena kupata huduma ya kawaida ya waandishi ndani ya White House.
Utawala wake ulidai kuwa baadhi ya taarifa zilizochapishwa na vyombo hivyo zilihusisha masuala ya usalama wa taifa, huku vyombo hivyo vikidai kuwa hatua hiyo ilikiuka haki zao za kikatiba.
Kwa mujibu wa uamuzi wa jaji, utawala wa Trump unatakiwa kurejesha press passes za waandishi wa vyombo hivyo na kusitisha utekelezaji wa marufuku hiyo kwa kipindi cha siku 14 wakati mchakato wa kesi ukiendelea.
Na Ashura Karimu
