HOFU YA MAPOROMOKO YA ARDHI, KAYA 40 CHOME, WILAYA YA SAME ZATAKIWA KUONDOKA

Na Ashrack Miraji Same Kilimanjaro 

Takribani kaya 40 katika kijiji cha Marieni, Kata ya Chome wilayani Same, zimeagizwa kuhama haraka katika maeneo hayo baada ya ardhi kusogea na kusababisha nyufa kubwa kujitokeza ardhini na kuleta uharibifu wa takribani nyumba 10 pamoja na kanisa moja, ambapo Serikali imesema hatua hiyo ni ya haraka kutokana na hatari ya kutokea kwa maafa katika eneo hilo lenye milima na miteremko kwa hofu ya kuporomoka kwa miamba.

Agizo hilo limetolewa baada ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) iliyopo chini ya wizara ya Madini kufanya utafiti na kubaini mabadiliko ya kijiolojia yanayoendelea chini ya ardhi katika eneo hilo na kusababisha nyufa na uharibifu huo. Mjiolojia kutoka GST Mjiolojia Mwandamizi Gabriel Mbogoni amesema utafiti umeonesha uwepo wa tabaka nene la udongo wa mfinyanzi ambalo lina maji, hali inayofanya ardhi kupoteza uimara na kuongeza uwezekano wa kusogea zaidi au kuporomoka.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, nyufa zimeonekana kuanzia maeneo ya juu ya mlima hadi katika mashamba na maeneo ya karibu na kanisa lililoharibiwa, huku baadhi ya miundombinu ya zege ikionekana kuinuka kutokana na msukumo unaotokea chini ya ardhi, amesema vipimo vya jiolojia na usumaku pia vimeonesha uwepo wa maeneo yenye tabaka kubwa la udongo wa mfinyanzi.

Mjiolojia huyo amesema hali hiyo ni matokeo ya mchakato wa muda mrefu wa kijiolojia, lakini shughuli za binadamu zimechangia kudhoofisha zaidi ardhi hiyo. Ametaja ukataji wa miti, kilimo na matumizi ya mifereji ya wazi ya umwagiliaji kuwa miongoni mwa mambo yanayofanya maji kubaki ardhini kwa muda mrefu na kupunguza uimara wa udongo wa mfinyanzi.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Makandeni, Marry Abuduel, amesema wamepokea maelekezo ya Serikali na wako tayari kuyatekeleza, lakini changamoto kubwa ni kupata maeneo salama ya kuwapeleka wananchi watakaohama aidha, ameomba TANESCO kuchukua hatua kuhusu baadhi ya nguzo za umeme katika maeneo hayo, akisema zimekuwa zikitumika kwa zaidi ya miaka 26, nyingine zimeanza kuoza na baadhi ya nyaya ziko karibu na ardhi yenye nyufa.

Mwananchi Elisa Mtera amesema hali hiyo imewaweka wananchi katika hofu kubwa kutokana na kuendelea kwa nyufa, huku familia zikikabiliwa na changamoto ya kutokuwa na maeneo ya kwenda endapo wataondoka, amesema wananchi, wazazi na watoto hawaishi kwa amani kutokana na hofu ya maafa, hasa wakati wa mvua za el nino, na kuiomba Serikali kuwapatia maeneo mbadala kwa haraka.

Akitoa maelekezo ya Serikali, Mkuu wa Wilaya Shikizi ya Same, Rukia Zuberi, amesema baada ya kusikiliza wataalamu, Serikali imebaini kuwa maeneo hayo si salama tena kwa makazi wala shughuli za maendeleo, hivyo wananchi wanapaswa kuondoka haraka huku akuwaagiza viongozi wa Halmashauri, kata na vijiji wana wajibu wa kuanza mchakato wa kutafuta maeneo salama ya makazi ya kudumu, huku wananchi wakitakiwa kuchukua hatua mapema za kuokoa maisha na mali zao.

 

Rukia amesema wananchi hawapaswi kusubiri maafa yatokee ndipo wachukue hatua, kwa kuwa maporomoko ya ardhi yanaweza kutokea wakati wowote na muda wake hauwezi kutabirika kwa usahihi. Amesisitiza kuwa tahadhari hiyo haiwahusu wakazi wa Chome pekee, bali wananchi wote wanaoishi katika maeneo yaliyobainishwa kuwa hatarishi, akiwataka kuondoka mapema wakati Serikali ikiendelea na mchakato wa kuwapatia maeneo salama ya kuishi.