Lamine Yamal: Sitaki Kuwa Bora Zaidi ya Pele na Messi

Global Publishers
September 23, 2026
0 views
0 Comments

Nyota wa FC Barcelona, Lamine Yamal, amesema hataki kujilinganisha na magwiji wakubwa wa soka kama Pele na Lionel Messi, bali anatamani kujenga historia yake mwenyewe na kukumbukwa kwa jina lake.

Akizungumza na gazeti la L’Équipe, Yamal amesema lengo lake ni kuandika historia yake katika soka bila kujaribu kuwa kama wachezaji waliomtangulia.

“Ninacheza ili kuandika historia. Sitaki kuwa bora kuliko Pele au Messi. Nataka kuwa Lamine Yamal na nikumbukwe kama Lamine Yamal. Natumaini nitakuwa miongoni mwa wachezaji wakubwa,” amesema Yamal.

Yamal tayari ameshinda mataji matatu ya La Liga akiwa na Barcelona, lakini amesema bado ana kiu kubwa ya mafanikio na angependa kuongeza idadi hiyo hadi kufikia mataji saba, nane au hata zaidi.

Kuhusu Ligi ya Mabingwa Ulaya, Yamal amesema bado hajafanikiwa kutwaa taji hilo na ana hamu kubwa ya kulibeba. Ameeleza kuwa endapo Barcelona itashinda, angependa kuendelea kupambana hadi kufikia hatua za mwisho na kushinda mataji matatu mfululizo, hasa akiwakabili wapinzani kama Paris Saint-Germain.

Kwa upande wa Ballon d’Or, Yamal amesema bado hajafikia malengo yake katika tuzo hiyo na anaamini mwaka unaofuata anaweza kuwa na nafasi kubwa zaidi. Endapo atashinda, amesema hilo litaongeza motisha kwake kutafuta mafanikio mengine.

Kwa ujumla, Yamal ameweka wazi kuwa hataki kuishi chini ya kivuli cha Messi au Pele bali anataka kujenga urithi wake mwenyewe na kuacha alama katika historia ya soka.

Na Tereza Muga