MWANZA; Serikali imeongeza bajeti ya mikopo na ruzuku kwa wanafunzi wa elimu ya juu hadi Sh 1.06 trilioni kwa mwaka wa masomo 2026/2027, fedha zinazotarajiwa kuwezesha wanafunzi wasiopungua 292,463.
Hayo yamesemwa leo Septemba 23 na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Dk Bill Kiwia, wakati akizungumza katika kikao kazi cha maofisa mikopo wa vyuo vya elimu ya juu na vya kati jijini Mwanza.
Amesema ongezeko hilo linaifanya miaka miwili mfululizo kuwa ya kuvunja rekodi katika bajeti na idadi ya wanufaika wa mikopo na ruzuku.

Dk Kiwia amesema katika mwaka wa masomo 2025/2026 zilitengwa Sh 916.7 bilioni, zilizowanufaisha wanafunzi 252,773.
Amesema mwaka wa masomo 2026/2027, serikali imetenga Sh1.06 trilioni, huku idadi ya wanufaika ikitarajiwa kufikia wasiopungua 292,463.
“Miaka hii miwili 2025/2026 na huu tunaelekea kuanza wa 2026/2027, imevunja rekodi kwa bajeti na wanufaika,” amesema Dk Kiwia.
Kwa mujibu wa Dk Kiwia, ongezeko hilo linaonesha jitihada za serikali katika kuwezesha vijana wenye sifa kumudu gharama za elimu ya juu na kupata taaluma mbalimbali kwa ajili ya kulitumikia Taifa.
