Shigongo Aipongeza TMDA Kudhibiti Dawa Bandia Nchini

Global Publishers
September 23, 2026
24 views
0 Comments

Mbunge wa Jimbo la Buchosa, Eric Shigongo, ameipongeza Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba nchini (TMDA), chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Adam Mitang’u Fimbo, kwa hatua zinazochukuliwa kudhibiti uingizaji na usambazaji wa dawa bandia nchini.

Katika taarifa iliyotolewa Septemba 22, 2026, TMDA imeeleza kuwa dawa bandia zimekuwa tishio kwa afya na maisha ya Watanzania, ikiwemo kuchangia usugu wa vimelea dhidi ya dawa, hali inayoweza kusababisha madhara makubwa kwa afya ya jamii.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa hivi karibuni TMDA imekamata shehena za dawa zenye thamani ya mamilioni ya shilingi, ambazo zimebainika kuwa na viashiria vya kutokuwa salama au kutokidhi viwango vinavyotakiwa.

Aidha, Shigongo ameiomba TMDA kuendelea kuimarisha ukaguzi katika maghala ya kuhifadhia dawa, pamoja na kwa wafanyabiashara na waingizaji wa dawa, ili kuhakikisha ubora na viwango vya dawa vinachunguzwa kabla hazijawafikia wananchi.

Pia, ameiomba Serikali kuendelea kuiwezesha TMDA kwa bajeti, watumishi na vitendea kazi vya kutosha ili kuimarisha udhibiti wa dawa zisizokidhi viwango nchini.