
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuna msukumo mkubwa kuelekea kufikiwa kwa makubaliano na Iran, lakini ameonya kuwa muda wa kufikia suluhu hiyo unaendelea kupungua.
Trump amesema hayo Jumanne, Septemba 22, 2026, wakati wa mkutano na viongozi kadhaa wa Mashariki ya Kati pembezoni mwa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) mjini New York.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Emir wa Qatar, Mfalme wa Jordan, Marais wa Uturuki na Syria, maafisa wa Misri pamoja na viongozi waandamizi wa serikali ya Marekani.
Trump amesema wajumbe wake, Steve Witkoff na Jared Kushner, walifanya mazungumzo na wapatanishi wa Iran siku hiyo, akidai kuwa upande wa Iran unawaheshimu wajumbe hao.
“Kuna msukumo mkubwa wa wao kufikia makubaliano. Hivyo ndivyo tunavyosikia kutoka kwa kila mtu,” Trump alisema.
Amesema uchumi wa Iran uko katika hali mbaya na kwamba anatumaini viongozi wa Iran watachukua hatua zitakazokuwa na manufaa kwa wananchi wake.
Trump pia amesema mpango wa nyuklia wa Iran umekuwa miongoni mwa changamoto kubwa ambazo utawala wake umejaribu kuzitatua mwaka huu.
Aidha, amedai kuwa operesheni za kijeshi na shinikizo la kiuchumi la Marekani zimeathiri kwa kiwango kikubwa uwezo wa Iran kijeshi na kiuchumi, huku akisema Marekani inaendelea kuiwekea Iran shinikizo ili ifikie makubaliano.
“Kutakuwa na wakati ambapo itakuwa imechelewa, na hatutakuwa na nafasi ya kuiruhusu iendelee kuishi kama taifa,” Trump alisema, akizungumzia hitaji la Iran kufikia makubaliano.
Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Trump kuzungumza katika UNGA na kutoa onyo kali kwamba anaweza kuchukua hatua zaidi dhidi ya Iran iwapo makubaliano hayatapatikana. Wakati huohuo, maafisa wa Iran wameeleza utayari wa kurejea katika diplomasia endapo Marekani itapunguza shinikizo la kijeshi na kuondoa vizuizi dhidi ya bandari za Iran.
