Global Publishers
September 22, 2026
0 views
0 Comments
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linamshikilia dereva wa TARURA Wilaya ya Dodoma, Sath John Masawa (31), kwa tuhuma za kumtishia dereva wa basi la SATCO kwa kutumia kitu kinachodhaniwa kuwa bastola.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, tukio hilo linadaiwa kutokea wakati Said Fadhili (54), dereva wa basi la SATCO lenye usajili T308 EME, akiwa anatoka kuweka mafuta katika kituo cha Total Energies.

Inadaiwa kuwa Masawa alimtishia Said kwa kitu hicho na kisha kumfuata kwa gari la TARURA lenye usajili STM 5806, aina ya Land Cruiser LX 70 Series, lililokuwa likiendeshwa na mtuhumiwa.
Baada ya kuripotiwa kwa tukio hilo, Jeshi la Polisi lilifika eneo la tukio na kumkamata Sath John Masawa. Baada ya upekuzi, ilibainika kuwa kitu alichokuwa nacho na kudhaniwa kuwa bastola hakikuwa silaha halisi, bali ni kitu kinachofanana na silaha.
Aidha, Jeshi la Polisi limebaini kuwa gari la TARURA lenye usajili STM 5806 lilikuwa halitumii namba zake za usajili halali, badala yake lilikuwa likitumia namba T 881 ENZ, ambazo ni za gari mali ya mtu mwingine.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linaendelea kumshikilia mtuhumiwa kwa ajili ya mahojiano na hatua zaidi za kisheria.
Jeshi la Polisi limetoa wito kwa madereva kuacha kutumia namba bandia za magari na kufanya vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa watumiaji wengine wa barabara, likisisitiza kuwa kufanya hivyo ni kosa kwa mujibu wa sheria.


