Wazazi sita ‘wabanwa’ kwa watoto kutokwenda shule
Simanjiro.Wazazi na walezi sita katika Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara, wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kushindwa kuhakikisha watoto wao wanahudhuria masomo shuleni.
Hatua hiyo imetangazwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Gracian Max Makota, jana Agosti 18, 2026, alipozungumza katika kikao cha baraza la madiwani la halmashauri hiyo.
Makota amesema hatua ya kuwafikisha wazazi hao mahakamani inalenga kuimarisha uwajibikaji wa wazazi na walezi katika kuhakikisha watoto walio katika umri wa kwenda shule wanahudhuria masomo kwa mujibu wa sheria na taratibu za elimu.
Amesema baadhi ya watoto wamekuwa wakikosa masomo mara kwa mara bila sababu za msingi, hali inayoweza kuathiri maendeleo yao kielimu na kuongeza uwezekano wa kuacha shule.
“Ninyi madiwani, hata wapiga kura wenu wakija kuwaomba dhamana kwa sababu ya kukamatwa kwa utoro wa watoto wao, msikubali kuwaunga mkono, kwani watazoea kuwazuia watoto kwenda shule,” amesema Makota.
Amewaasa madiwani kuacha tabia ya kuwatetea wazazi wasiotaka watoto wao kwenda shule, kwani inachangia kuongeza utoro na kushuka kwa kiwango cha taaluma shuleni.
“Bahati nzuri, watoto wa jamii ya kifugaji wana akili mno shuleni. Sasa madiwani, msiunge mkono utoro, waelezeni kabisa wapiga kura wenu kuwa elimu ni maendeleo,” amesema.
Diwani wa Naberera, Marco Munga, amesema wazazi na walezi wa eneo hilo wameshapitisha sheria ndogo ya kutoa Sh50,000 na faini ya Sh200,000 mtoto asipokwenda shule.
Munga amesema faini hiyo imelenga kudhibiti utoro kwa kuwabana wazazi na walezi wa wanafunzi kuwatoza fedha ili watoto wao waende shule, wasiende kuchunga mifugo.
“Suala la kudhibiti mimba shuleni, tumewaelekeza wazazi na walezi kuwapima mabinti mara kwa mara ili wazingatie masomo na kuachana na tabia mbaya,” amesema Munga.
Diwani wa Mirerani, Salome Mnyawi, amesema inatakiwa kujengwa shule nyingine ya msingi ili kuepuka msongamano wa shule mbili za Serikali kwenye eneo hilo.
“Shule zetu mbili za msingi, Songambele na Tanzanite, hivi sasa zina mrundikano mkubwa wa wanafunzi, hivyo tunapaswa kujenga shule nyingine ya msingi,” amesema Salome.
Diwani wa Ngorika, Albert Msole, amesema miundombinu inapaswa kuboreshwa katika Shule ya Sekondari Nyumba ya Mungu ili ikidhi vigezo vya kupokea wanafunzi wa kidato cha tano.
“Mwenyekiti, pamoja na madarasa ya Shule ya Sekondari Nyumba ya Mungu ambayo tuliyojenga, tunapaswa kuboresha miundombinu ili kukidhi vigezo vya elimu ya juu,” amesema Msole.

