Wakulima wa zao la mahindi mkoani Njombe wameiomba serikali kuwapa vibali vya kuuza mahindi nje ya nchi kutokana na kuporomoko kwa soko la ndani ambalo litasababisha kupata hasara kubwa ukilinganisha na bei za uzalishaji.
Wakiwa kwa mkuu wa mkoa wa Njombe baadhi ya wakulima wakubwa wa mahindi toka wilayani Ludewa Akiwemo George Mkinga wamesema kitendo cha serikali kupitia wakala wa hifadhi ya chakula cha Taifa NFRA Kutangaza kuanza kununua mahindi hayo kwa shilingi 450 kwa Kilo badala ya shilingi 700 hadi 1000 kama misimu iliyopita kinawapa ugumu ukizingatia kuna hatari ya mvua kubwa za El nino ambazo zinaweza kuharibu mazao hayo.
Wamesema mwaka huu hususani wilaya ya Ludewa wamevuna mahindi mengi kiasi cha mkulima mmoja kuvuna hadi gunia 8000 lakini hakuna maghala ya kuhifadhia mazao na kuyauza kwa bei hiyo watapata hasara kubwa hivyo wamemuomba mkuu wa mkoa awafikishie kilio chao kwa Rais Samia.
Viongozi wa wilaya ya Ludewa akiwemo Mhe.Olivanus Thomas mkuu wa wilaya na Mkurugenzi Sunday Deogratias wamesema wameshafanya mazungumzo na wakulima wao na kuanza kuchukua hatua mbalimbali zikiwemo za kutafuta wanunuzi katika maeneo mengine ili kuona namna ya kuwasaidia wakulima hao.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Njombe Antony Mtaka ameahidi kufanya mawasiliano na Waziri wa Kilimo Kuona namna ya kuelekeza nguvu ya kununua mahindi hususani katika wilaya ya Ludewa ambayo imetajwa kuvuna mahindi mengi hasa katika vijiji vya Ibumi na Amani.
Wanasema kwa ekari moja inayotumia zaidi ya shilingi milioni moja kulima zao la mahindi unaweza kupata shilingi laki saba baada ya mavuno ikiwa hasara ni takribani shilingi laki tatu endapo mahindi yatauzwa kwa shilingi 450 kwa Kilo.




