JKT Yaweka Mkazo Uzalendo wa Kidijitali, Mabele Atoa Maagizo kwa Vijana – Video

Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Rajabu Mabele, amesema somo la Uzalendo na Uzalendo wa Kidijitali katika silabasi za mafunzo ya JKT litaendelea kuboreshwa ili kuwaelimisha vijana kuhusu umuhimu wa kutumia mitandao ya kijamii kwa usahihi na kwa manufaa ya Taifa.

Meja Jenerali Mabele amesema hayo Septemba 18, 2026, wakati akifunga mafunzo ya awali ya kijeshi kwa vijana wa Mujibu wa Sheria kupitia Operesheni Linda Amani na vijana wa kujitolea kupitia Operesheni Nishati Safi katika Kikosi cha Kanembwa JKT, mkoani Kigoma.

Amesema mafunzo hayo yana nafasi kubwa katika kuwajenga vijana kuwa wazalendo, wenye nidhamu na wanaotambua wajibu wao katika ujenzi na ulinzi wa Taifa, ikiwemo matumizi sahihi ya teknolojia na mitandao ya kijamii.

Akiwasilisha salamu za Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Brigedia Jenerali Lawrence Lugenge, Meja Jenerali Mabele amewapongeza vijana hao kwa kukubali kujiunga na JKT na kuwataka kuyaendeleza kwa vitendo maarifa na mafunzo waliyoyapata.

Kwa upande wake, Mkuu wa Tawi la Mafunzo JKT, Brigedia Jenerali Peter Mnyani, amewapongeza wahitimu hao kwa kuwa watiifu na kuzingatia taratibu wakati wote wa mafunzo.

Naye Mkuu wa Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar, Kanali Makame Daima, amewataka vijana hao kuendelea kuulinda na kuuenzi Muungano wa Tanzania.

Akitoa taarifa ya mafunzo hayo, Kamanda wa Kikosi cha Kanembwa JKT, Kanali Mantage Nkombe, amesema vijana wote waliohitimu wamepatiwa mafunzo ya kinadharia na vitendo kwa kuzingatia silabasi husika na wamefaulu kwa viwango vinavyokubalika ndani ya JKT.

Zoezi la kufunga mafunzo ya JKT lilianza rasmi Septemba 8, 2026 katika vikosi mbalimbali vya mafunzo vya JKT. Kwa mara ya kwanza, mafunzo hayo yamefanyika kwa kuwakutanisha vijana kutoka makundi mawili, ambao ni vijana wa kujitolea kupitia Operesheni Nishati Safi na vijana wa Mujibu wa Sheria.