Jamhuri yafunga ushahidi kesi ya Lissu
Dar es Salaam. Jamhuri imefunga ushahidi wake katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Lissu,
Jamhuri imefunga ushahidi huo leo Jumatatu Agosti 17, 2026 baada ya kuwaita mashahidi 17 kati ya 30 waliokuwa wameorodheshwa.
Katika kesi hiyo Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kusudio la kuzuia kufanyika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kwa kutamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi mkuu wa Serikali ya Tanzania, kuwa:-
“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko… kwa hiyo tunaenda kikinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli… tunaenda kukinukisha vibaya sana…”
Kesi hiyo inasikilizwa na Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, Jaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, ilipangwa kuendelea leo kwa ushahidi wa upande wa Jamhuri.
Hata hivyo baada ya kesi kuitwa Jamhuri kupitia mwendesha mashtaka Wakili wa Serikali Mkuu Ajuaye Nzegeli ameieleza Mahakama kuwa baada ya kupitia ushahidi uliokwishawasilishwa na kuangalia ushahidi wa mashahidi waliosalia wameona ushahidi waliokwishawasilishwa unatosheleza.
“Hivyo tunapenda kuitaarifu Mahakama hii tukufu kuwa upande wa Jamhuri unafunga ushahidi wake kwa mashahidi 17”, amesema Wakili Nzegeli.
Baada ya Jamhuri kufunga ushahidi wake sasa kesi imeingia katika hatua ya pili ambapo pande zote zinawasilisha hoja kuishawishi mahakama kama mshtakiwa kwa ushahidi huo ana kesi ya kujibu au la.
Kwa sasa ameanza mshtakiwa Lissu kuwasilisha hoja zake kuishawishi Mahakama kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuonesha kuwa kuna kesi ya kumfanya ajitetee, kabla ya upande wa mashtaka kujibu hoja hizo kuionesha Mahakama kuwa imeweza kujenga kesi kiasi cha kumlazimu mshtakiwa kujitetea kabla ya kutoa hukumu.

