BALOZI SIRRO AHIMIZA WATANZANIA KUKATA BIMA

 

Na Fadhili Abdallah,Kigoma 

Mkuu wa mkoa Kigoma  Balozi Simon Sirro  amewataka Watanzania kubadili mtazamo wao kuhusu bima na kuanza kuiona kama sehemu ya maandalizi ya maisha badala ya kuichukulia kuwa gharama isiyo na umuhimu.

Balozi Sirro alisema hayo wakati akizindua kampeni ya utoaji elimu na uhamasishaji jamii kujiunga na huduma za bima za maisha na mali zinazotolewa na Shirika la Bima la Taifa (NIC) ambapo alibainisha kuwa bima ya maisha na mali ni muhimu kwa maisha ya Watanzania kabla hawajapata majanga.

Katika hotuba ya Mkuu huyo wa mkoa iliyotolewa na  Mkuu wa wilaya Kigoma,DkRashid Chuachua alisema kuwa  wananchi wanapaswa kuhakikisha wanaweka mipango ya kulinda maisha yao, familia, mali na shughuli za uzalishaji kwa kuchagua aina ya bima inayokidhi mahitaji yao kutoka NIC.

Awali Mkurugenzi wa idara ya mawasiliano  na masoko wa shirika hilo, Karim Meshack alimesema kuwa elimu  na ufahamu duni wa umuhimu wa bima umechangia idadi kubwa ya watanzania kushindwa kukata bima za maisha na mali  na hivyo kuathirika yanapotokea majanga ambapo kwa sasa ni asilimia tano tu ya watanzania ndiyo wamejiunga na huduma hiyo.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa  changamoto kubwa ni baadhi ya wananchi kutotambua kuwa bima ni kinga muhimu ya maisha, mali na shughuli zao za kiuchumi, badala yake wengi huanza kufikiria kuhusu bima baada ya kukumbwa na ajali au kupata hasara ambapo alisema kuwa bima inaweza kumsaidia mtu, familia au mfanyabiashara kukabiliana na athari za kifedha zinazoweza kujitokeza baada ya kutokea tukio lisilotarajiwa.

Kwa sasa  alisema kuwa katika awamu hii ya kampeni hiyo kwa mikoa ya Magharibi na kanda ya ziwa itakayochukua siku 12 alisema kuwa watafika maeneo mbalimbali ya mkoa Kigoma kampeni inayojulikana kama NIC Kitaa na kwamba bima ya mali na maisha ni muhimu kwa maisha ya Mtanzania kabla na anapopata majanga.

Mwisho.