
Msanii Juma Jux ametoa tamko kwa umma akikanusha madai yanayosambaa yakimuhusisha kuwa baba wa mtoto wa mtu fulani, akisema taarifa hizo hazina ukweli na sasa suala hilo limefikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Kupitia tamko hilo, Jux amesema amekuwa akifuatilia suala hilo kwa utulivu bila kulipa uzito, kwa kuwa awali aliona halina msingi wala halistahili kupewa nafasi, lakini ameamua kulizungumzia baada ya madai hayo kuendelea kuhusisha jina lake, familia yake, biashara zake na taswira aliyoijenga kwa miaka mingi kwa jasho na kazi kubwa.
Jux amesema suala hilo liliwahi kujitokeza hapo nyuma, ambapo kwa kutaka kujiridhisha kuhusu chanzo cha madai hayo, alichukua hatua ya kumtafuta mhusika mwenyewe ili kufahamu ni kwanini alikuwa akisema alichokuwa amekisema hapo awali.

Kwa mujibu wa Jux, mhusika huyo alithibitisha kwa maneno na kwa sauti yake kuwa hakuwahi kukutana naye kimwili wala kuwa na mahusiano ya kimapenzi naye.
Aidha, Jux amesema mhusika huyo alimuomba asilipe uzito suala hilo, akieleza kuwa madai hayo yalitokana na maoni ya baadhi ya mashabiki waliokuwa wakimfananisha mtoto huyo na Jux, jambo lililopelekea baadhi yao kuanza kumhusisha kuwa baba wa mtoto.
Hata hivyo, Jux amesema madai hayo yameibuka tena na sasa yamechukua mwelekeo tofauti, hali iliyomfanya kuchukua hatua za kisheria.

Amesema suala hilo kwa sasa lipo mikononi mwa vyombo vya sheria, huku akieleza kuwa hatua zaidi zitachukuliwa dhidi ya mhusika.
Jux pia ametoa rai kwa vyombo vya habari na watu mbalimbali kuepuka kusambaza taarifa za kupotosha bila kuwa na uhakika wa ukweli wake, akisisitiza kuwa taarifa zisizo na ukweli zinaweza kuathiri jina, familia na biashara ya mtu.

Katika tamko lake, Jux amesema amejenga jina lake, brand na biashara zake kwa miaka mingi kupitia kazi, nidhamu na kujituma, hivyo mtu yeyote anayechagua kuhusisha jina lake, familia yake au biashara zake na madai yasiyo ya kweli, atalazimika kuwajibika kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wake, Jux amesema amechagua kubaki katika utulivu na kusimamia ukweli, huku akiacha hatua zaidi zichukuliwe kupitia njia sahihi za kisheria.
“Kwa upande wangu, nimechagua utulivu, ukweli na hatua sahihi za kisheria,” Jux amesema katika tamko lake.
STORI NA Na DIDAS DIDAS | GPL -TUDACO
