Kwanini maboresho ya mifumo NMB ni muhimu kwako

Dar es Salaam. Ongezeko la wateja kutoka milioni 1.8 mwaka 2011 hadi zaidi ya milioni 10 kwa sasa limetajwa kuwa moja ya sababu iliyoifanya Benki ya NMB kufanya maboresho ya mfumo mkuu wa benki ili kuendana na mahitaji hayo.

Maboresho hayo ni zaidi ya kubadilisha mfumo wa kiteknolojia unaolenga kuongeza kasi, usalama, uthabiti na uwezo wa benki kutoa huduma mpya kwa wateja.

Akizungumza katika mahojiano maalumu leo Alhamisi, Agosti 20, 2026, Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna amesema mfumo huo umejengwa kuendana na ukuaji wa benki na kuifanya teknolojia isiwe kikwazo katika utoaji wa huduma.

“Kilichofanyika si uboreshaji wa mfumo pekee bali ni uwekezaji katika usalama, uthabiti, kasi, ubunifu na uwezo wa NMB kukua pamoja na Watanzania. Mfumo mpya umejengwa kuhimili ukuaji wa benki, kuongeza ufanisi wa miamala na kuwezesha kizazi kipya cha huduma za kidijitali na kifedha,” amesema.

Kwa sasa NMB ina zaidi ya matawi 250, mawakala zaidi ya 80,000, ATM zaidi ya 750 na zaidi ya QR Codes 130,000 zinazotumika kupokea malipo; ukuaji uliofanya mfumo uliokuwa ukitumika tangu mwaka 2011 kutotosheleza mahitaji ya benki hiyo kwa sasa na miaka ijayo.

“NMB sasa imehamia kwenye mfumo mpya wa Core Banking unaolenga kuongeza uwezo wa kushughulikia miamala, kuimarisha uthabiti wa huduma na kuwezesha benki hiyo kuanzisha bidhaa mpya za kifedha,” amesema.

Kwa mteja, umuhimu wa maboresho hayo unatarajiwa kuonekana katika huduma zenye kasi na uthabiti zaidi, pamoja na kuimarika kwa huduma za kidijitali kupitia NMB Mkononi, USSD, ATM na mawakala.

Zaipuna amesema mfumo huo pia utawezesha benki kuanzisha bidhaa na huduma mpya kwa haraka zaidi, huku ukiboresha usalama na ufanisi wa miamala.

“Kwa mteja, maboresho haya yanamaanisha huduma za kasi zaidi, salama zaidi, zinazotegemeka zaidi na zinazoweza kuendana kwa karibu zaidi na mahitaji yake,” amesema.

Kwa wafanyabiashara, kampuni na taasisi, mfumo huo umeongeza uwezo wa kushughulikia miamala mingi kwa wakati mmoja, malipo na ukusanyaji wa fedha pamoja na huduma za mishahara.

“Kwa kampuni kubwa mfumo huu una uwezo wa kuratibu ulipaji wa mishahara kwa zaidi ya wafanyakazi 20,000 wa kampuni moja,” amesema.

Zaipuna amesema hadi maboresho hayo yanafanyika kulikuwa na maandalizi ya zaidi ya miaka miwili tangu mwaka 2023 na ulihusisha majaribio ya mara kwa mara, uhakiki wa mifumo, tathmini za vihatarishi na ushirikishwaji wa wataalamu wa ndani na nje ya benki.

Hatua ya mwisho ya uhamishaji wa mfumo ilianza Julai 31, 2026,  baadhi ya huduma zilisitishwa kwa muda ili kuruhusu uhamishaji wa taarifa kufanyika kwa usalama.

“Hatukuchagua njia rahisi, tulichagua njia salama na yenye uwajibikaji zaidi kwa wateja wetu,” amesema Zaipuna.

Amesema mfumo huo mpya unaweka msingi wa utekelezaji wa Mpango Mkakati wa NMB wa 2026-2030, unaolenga kuifanya benki hiyo kuwa ya kisasa, salama na inayoendeshwa zaidi na teknolojia.

“Hatua hii inaweka msingi muhimu wa utekelezaji wa Mpango Mkakati wa NMB 2026-2030, unaolenga kuendeleza NMB kuwa benki ya kisasa, salama, inayozingatia mteja, inayoendeshwa na teknolojia na yenye mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania,” amesema.