Dar es Salaam. Mkoa wa Dar es Salaam umeongoza kwa matumizi na idadi ya vifaa vya kujipima maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) vilivyosambazwa nchini mwaka 2025 huku zaidi ya vifaa 330,000 vikifikishwa kwa wananchi.
Takwimu hizo ni kwa mujibu wa Ripoti ya Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini (NASHCoP) ya mwaka 2025. Mpango huo upo chini ya Wizara ya Afya.
Takwimu hizo zinaonesha kati ya vifaa 2,494,398 vya kujipima VVU vilivyosambazwa nchini mwaka huo, Dar es Salaam ilipokea vifaa 330,351, sawa na takribani asilimia 13 ya vifaa vyote vilivyosambazwa.
Dar es Salaam ilifuatiwa na Mbeya iliyosambaziwa vifaa 221,963, Tabora 200,784, Pwani 188,351 na Tanga 179,533.
Huduma ya kujipima VVU, maarufu kama HIV self-testing, imekuwa ikilenga kuongeza wigo wa upimaji kwa kuwapa wananchi fursa ya kujua hali zao kwa faragha na urahisi zaidi, hususan wanaume na vijana ambao wanaweza kukumbana na vikwazo vya kufika katika vituo vya afya.
Kwa mujibu wa NASHCoP, tafiti pia zimeonesha matumizi ya vifaa hivi kuwa makubwa zaidi maeneo ya mijini kuliko vijijini.
Kwa ujumla, kati ya vifaa 2,494,398 vilivyosambazwa nchini, 2,118,462 vilirejeshwa pamoja na majibu ya vipimo, sawa na karibu asilimia 85.
Hata hivyo, Dar es Salaam, licha ya kuongoza kwa idadi ya vifaa vilivyosambazwa, haikuwa miongoni mwa mikoa yenye kiwango cha juu zaidi cha kurejesha majibu.
Katika vifaa 330,351 vilivyosambazwa jijini, 269,389 vilirejeshwa pamoja na majibu, sawa na takribani asilimia 82.
Takwimu hizo pia zinaonesha vifaa 1,292 vilirejeshwa vikiwa na majibu ya reactive, yanayoashiria uwezekano wa maambukizi ya VVU.
Majibu ya reactive kwenye kipimo cha VVU maana yake ni kwamba kipimo kimeonesha ishara inayoweza kuashiria uwepo wa maambukizi ya Ukimwi.
Kati ya watu hao, 452 pekee walithibitishwa kuwa na maambukizi na mtoa huduma za afya, sawa na asilimia 35 ya majibu ya reactive yaliyorekodiwa Dar es Salaam.
Hali hiyo inaibua maswali kuhusu hatua zinazochukuliwa baada ya mtu kupata majibu ya reactive kupitia kipimo cha kujipima, kwa kuwa kipimo hicho hakitoshi pekee kuthibitisha mtu kuwa na VVU.
Kwa mujibu wa uchambuzi wa takwimu za mwaka 2025, kitaifa kulikuwa na majibu 10,867 ya reactive kutoka kwenye vifaa vilivyorejeshwa, lakini watu 5,130 pekee walithibitishwa kuwa na maambukizi na watoa huduma za afya, sawa na asilimia 47.
Tofauti kubwa pia imeonekana kati ya mikoa. Kilimanjaro ilikuwa na kiwango cha uthibitisho cha asilimia 100, Mwanza asilimia 86, Shinyanga asilimia 80 na Arusha asilimia 77. Kwa upande mwingine, Mtwara ilikuwa na asilimia nane, Morogoro asilimia 16, Mbeya 19 na Lindi asilimia mbili.
Wakati huohuo, baadhi ya mikoa ilirekodi idadi ya watu waliothibitishwa kuwa na HIV iliyozidi idadi ya majibu ya reactive yaliyotokana na vifaa vya kujipima. Iringa, kwa mfano, ilikuwa na majibu 42 ya reactive lakini watu 49 walithibitishwa kuwa na HIV, huku Manyara ikiwa na majibu 63 ya reactive dhidi ya watu 91 waliothibitishwa.
Uchambuzi unaonesha tofauti hizo zinaweza kusababishwa na makosa ya uingizaji wa taarifa, kutokulingana kwa vipindi vya usambazaji wa vifaa na utoaji wa majibu, pamoja na vipimo vya uthibitisho vinavyofanyika katika vituo tofauti kutounganishwa na kituo kilichosambaza kifaa cha kujipima.
Changamoto nyingine ni kukosekana kwa vitambulisho vya kipekee vinavyoweza kumfuatilia mtu kutoka hatua ya kujipima, kwenda kwenye kipimo cha uthibitisho na hatimaye kuunganishwa na huduma za matibabu.
Watafiti wamekuwa wakionesha HIV self-testing inaweza kusaidia kupunguza baadhi ya vikwazo vinavyowafanya wanaume kutofika kupima, ikiwamo suala la faragha, unyanyapaa na urahisi wa kupata huduma.
Hata hivyo, takwimu za mwaka 2025 zinaonesha pamoja na kuongezeka kwa usambazaji wa vifaa, bado kuna haja ya kuimarisha mfumo wa kufuatilia mtu anayepata majibu ya reactive hadi anapofanya kipimo cha uthibitisho na kupata huduma stahiki.


