Dkt Mwigulu: Serikali Kuendelea Kushirikiana Na Taasisi Za Dini Katika Maendeleo Ya Taifa – Video

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu taasisi za dini likiwemo kanisa Katoliki katika kuimarisha huduma za kijamii, maendeleo na ustawi wa wananchi, akisisitiza kuwa mchango wa taasisi za dini ni sehemu muhimu ya safari ya maendeleo ya Tanzania.

Dkt. Mwigulu ameyasema hayo leo Jumapili, Agosti 30, 2026, katika maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 25 ya Jimbo Katoliki la Mpanda, yaliyofanyika mkoani Katavi, ambapo amesema Serikali inatambua mchango wa Kanisa Katoliki katika maendeleo ya nchi, hususan katika sekta za elimu, afya na huduma za kiroho.

“Serikali inatambua mchango wa Kanisa na baba Askofu. Kila tunapotaja maendeleo ya nchi yetu, kuanzia mwanzo mpaka hapa tulipofika, hatuwezi kuyataja kwa kina maendeleo hayo bila kutaja mchango wa Kanisa.”

Amesema ushirikiano kati ya Serikali na Kanisa umeendelea kuwa muhimu katika kuhakikisha huduma za kijamii na shughuli za maendeleo zinaimarika, akisisitiza kuwa milango ya Serikali itaendelea kuwa wazi kwa Kanisa na taasisi nyingine za dini katika masuala yanayolenga ustawi wa wananchi.

“Niwahakikishie Serikali itaendelea kushirikiana na Kanisa na popote pale mlipo na jambo msisite, milango yetu iko wazi ili tuweze kuhakikisha kwamba tufanye jambo lolote linalotufurahisha.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa maelekezo kwa viongozi wa Mkoa wa Katavi na mamlaka husika kuharakisha utekelezaji wa miradi ya barabara, maji na umeme, akisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kupata huduma hizo kwa wakati.

Amesema maandalizi ya kukabiliana na uwezekano wa kutokea kwa El Niño yanapaswa kwenda sambamba na hatua za vitendo, ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa mifereji na madaraja ili kupunguza athari za mafuriko.

Kuhusu huduma za maji, Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Maji na wahusika wa mradi wa maji Mpanda kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo ifikapo Desemba 2026, huku akisisitiza pia kuharakishwa kwa miradi ya barabara inayounganisha Katavi na mikoa jirani.