Skip to content
-
Subscribe to our newsletter & never miss our best posts. Subscribe Now!
Habarimpya

Habari Mpya Kilasiku

Habarimpya

Habari Mpya Kilasiku

  • Home
  • Sample Page
  • Home
  • Sample Page
Close

Search

  • https://www.facebook.com/
  • https://twitter.com/
  • https://t.me/
  • https://www.instagram.com/
  • https://youtube.com/
Subscribe
Habari

Shekilango ilivyopata sura mpya baada ya mabasi kuondolewa

By admin
August 18, 2026 3 Min Read
Comments Off on Shekilango ilivyopata sura mpya baada ya mabasi kuondolewa

Dar es Salaam. Kwa muda mrefu, eneo la Shekilango, pembezoni mwa Barabara ya Morogoro kuelekea Magomeni, Dar es Salaam, lilizoeleka kuona msongamano wa mabasi ya kampuni mbalimbali yakiwa yameegeshwa na kupakia abiria wanaosafiri kwenda mikoa tofauti nchini. Sasa eneo hilo limebadilika baada ya mabasi hayo kuondolewa.

Mabasi hayo hayaonekani tena yakiwa yameegeshwa katika eneo hilo kama ilivyokuwa awali, isipokuwa yanapita kuelekea maeneo mengine au kuegeshwa kwa muda mfupi kupakia mizigo na abiria kabla ya kuondoka.

Hata hivyo, ofisi za kampuni za mabasi zilizolipamba eneo hilo kiasi cha kulifanya lionekane kama kituo cha mabasi bado zimefunguliwa na zinaendelea na shughuli za ukatishaji tiketi kwa abiria wanaosafiri kwenda mikoa mbalimbali.


Mawakala nao bado wanaendelea kuzengeazengea huku na kule  kusaka abiria kama ilivyo kawaida yao.

Nje ya baadhi ya ofisi hizo, ikiwemo za mabasi ya Katarama, BM, Happy Nation na Abood, ambazo mara nyingi hufurika abiria na kuwapo pilikapilika za hapa na pale, vifurushi vya mizigo ya abiria vimepangwa huku vikiwa vimeandikwa majina ya wahusika.

Hali hiyo inaonyesha kuwa shughuli za usafirishaji bado zinaendelea katika eneo hilo, licha ya mabasi kuondolewa kwenye vituo vyao.

Basi la kampuni ya Abood likiwa limesimama katika kituo chake kilichopo eneo la Shekilango, karibu na Ubungo Plaza, eneo hilo aghalabu hujaa mabasi mengi yakiwa yamejipanga ya kampuni hiyo, hasa nyakati za asubuhi na jioni kupakia abiria kwenda mikoa tofauti.

Mabadiliko hayo yamekuja baada ya tamko la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alilolitoa Agosti 11, 2026 ambapo  aliwataka wamiliki wa mabasi kuondoa magari yao katika vituo vilivyopo maeneo hayo na kuanza kutumia Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli, Mbezi Luis.

Kwa mujibu wa Chalamila, taarifa alizonazo zinaonyesha kuwa ni kampuni sita pekee zilizokuwa na vibali vya kuendesha vituo vya mabasi katika eneo hilo.

Alisema kampuni hizo zitaendelea na shughuli zake hadi vibali vyao vitakapoisha, kisha zitaungana na nyingine katika Kituo cha Mabasi cha Magufuli.

Chalamila alidai kuwa kuendelea kwa mabasi hayo kupakia abiria katika eneo hilo au kuja katikati ya Jiji la Dar es Salaam kunasababisha foleni na kuwaondolea watoa huduma wengine wa usafiri wateja zikiwamo daladala, bodaboda na mabasi ya mwendokasi.

Agizo hilo halikuwafurahisha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), ambao walidai kuwa hatua hiyo ilichukuliwa bila kuwashirikisha, hivyo hawakutendewa haki.

Hata hivyo, walisema hawana mpango wa kushindana na Serikali na kuahidi wanamtafuta Chalamila wafanye naye mazungumzo na kutoa tamko lao.

Mwananchi ilitembelea eneo hilo leo, Jumanne Agosti 18, 2026, kujionea hali ilivyo baada ya utekelezaji wa maelekezo hayo na kushuhudia mabadiliko makubwa ya mandhari.

Tofauti na ilivyozoeleka, eneo hilo sasa halina msongamano wa mabasi yaliyokuwa yakishusha na kupakia abiria. Ingawa, shughuli ndani ya ofisi za kampuni hizo zinaendelea kama kawaida.

Abiria bado wanaonekana kufika katika ofisi hizo kukata tiketi, huku mawakala wakizunguka huku na kule kuwatafuta wasafiri kwa ajili ya safari za mikoa mbalimbali.

Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi wa Habari kwa Umma wa Taboa, Mustapha Mwalongo, amesema wameutekeleza uamuzi huo, ingawa bado wanaendelea kutafuta nafasi ya kukutana na mkuu wa mkoa ili kuzungumza kuhusu suala hilo.

“Tangu Agosti 13 hadi sasa, nazungumza na wewe tunafanya jitihada za kumtafuta mkuu wa mkoa ili tuzungumze naye kuhusiana na jambo hili, lakini hatujafanikiwa. Barua tulishatuma. Naamini tukishafanya mazungumzo naye tutatoa msimamo wetu,” amesema Mwalongo.

Author

admin

Follow Me
Other Articles
Previous

RAIS WA KONGO MHE FELIX ANTOINE APOKELEWA NA RAIS DKT SAMIA IKULU NDOGO ZANZIBAR

Next

TMA yatahadharisha mvua, reli hatarini

Recent Posts

  • Serikali yatoa siku nane kwa wazalishaji saruji kushusha bei
  • Mchengerwa ataja vipaumbele sita kupunguza vifo vya mama, mtoto
  • Babu adai kupigwa ngwara na mwalimu Bahi
  • Kibwagizo cha wimbo wa ‘kilio cha mtu mzima’ kilivyotumika kesi ya ardhi
  • Mwili wa mtoto wa miaka saba wakutwa shimoni Tabora

Recent Comments

  1. A WordPress Commenter on Hello world!

Archives

  • August 2026

Categories

  • Habari
  • Magazeti
  • Michezo
Copyright 2026 — Habarimpya. All rights reserved. Blogsy WordPress Theme