Rukwa. Maonyesho ya sekta ya uvuvi yameanza kuleta matokeo chanya kwa kuwaunganisha wavuvi, wanawake, wasindikaji, wawekezaji na wanunuzi, hatua inayowawezesha kupata masoko mapya na kuongeza thamani ya bidhaa zao.
Mtaalamu wa masuala ya uvuvi na maendeleo ya jamii, Profesa Esther Ishengoma, amesema maonyesho hayo yamekuwa jukwaa muhimu kwa makundi ambayo hayajapata nafasi ya kutosha katika mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Agosti 16, 2026, Profesa Ishengoma amesema lengo kuu la maonyesho hayo ni kuwawezesha wavuvi, hasa wanawake wanaojihusisha na usindikaji na uuzaji wa bidhaa za uvuvi, kukutana moja kwa moja na wanunuzi, wawekezaji na wasindikaji wengine.
“Lengo letu kuu lilikuwa kuwapa fursa wavuvi, hasa wanawake wanaojihusisha na usindikaji na uuzaji wa bidhaa za uvuvi, waweze kuonyesha bidhaa zao moja kwa moja kwa wanunuzi na wawekezaji bila kupitia mawakala,” amesema.
Amesema wanawake na wavuvi wadogo wana mchango mkubwa katika usalama wa chakula na uendelevu wa rasilimali za uvuvi, licha ya kukabiliwa na changamoto za masoko.
“Tuliamua kuwapa nafasi kwa sababu ndio walio wengi katika sekta, lakini pia ndio wanaokabiliwa na changamoto kubwa zaidi za masoko. Mwanamke anapopata soko zuri, anaweza kuboresha lishe ya familia nzima. Mvuvi anapopata mkataba mzuri, anapunguza uvuvi haramu kwa sababu anakuwa na kipato cha uhakika,” amesema.
Kwa mujibu wa Profesa Ishengoma, maonyesho hayo tayari yameanza kuleta matokeo, yakiwemo baadhi ya washiriki kupata wateja wa hoteli, mikataba ya kusambaza bidhaa madukani na kukutana na taasisi za fedha na zinazotoa mafunzo ya uongezaji thamani.
Amesema baadhi ya wanawake wamepata ujuzi wa ufungaji na ubora wa bidhaa, huku wengine wakianzisha vikundi vya uzalishaji ili kuongeza uwezo wa kupata masoko makubwa.
FISH4ACP yaongeza thamani
Programu ya FISH4ACP ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) ni miongoni mwa mipango inayosaidia kuimarisha uwezo wa wadau wa sekta ya uvuvi nchini.
Programu hiyo inalenga kuifanya minyororo ya thamani ya uvuvi na ufugaji wa viumbe wa majini katika nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki kuwa endelevu, ikitekelezwa na FAO na washirika wake kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya na Wizara ya Shirikisho ya Ujerumani ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (BMZ).
Kupitia ushirikiano na Wizara ya Uvuvi, FISH4ACP imekuwa ikiwasaidia wasindikaji wadogo kupata mafunzo kuhusu usafi, ubora wa bidhaa na taratibu za kupata vibali vya kusafirisha mazao nje ya nchi.
Wanawake na vijana katika mwambao wa Ziwa Tanganyika mkoani Rukwa, Katavi na Kigoma wamewezeshwa kuanzisha shughuli za kuongeza thamani, ikiwemo usindikaji wa dagaa, kukaanga samaki kwa teknolojia safi na kufungasha bidhaa kwa viwango vinavyokubalika katika masoko ya kimataifa.
Mgeni Lubinsha wa Kata ya Kabwe, Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, ambaye ni mvuvi na mchakataji wa mazao ya majini, amesema, “Tulikuwa tunategemea soko la mtaani. Baada ya mafunzo na kushiriki maonyesho, sasa nina oda kutoka mataifa mbalimbali, ikiwemo Kenya. Haya ni mabadiliko makubwa kwetu.
Amesema awali dagaa walikuwa wakianikwa chini na kuuzwa kwa bei ndogo, lakini sasa wanatumia vifungashio bora, teknolojia za kisasa za ukaushaji na vikundi vya wanawake vinavyosindika dagaa kuwa unga na bidhaa za lishe.
Mdhibiti Ubora wa Masoko ya Mazao ya Uvuvi na mtoa leseni za kusafirisha mazao ya uvuvi nje ya nchi, Theresia Malobya, amesema leseni hizo ni muhimu katika kukuza biashara na uchumi wa ndani.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wavuvi, Francis Lubavu, amesema baada ya wanachama wake kushiriki maonyesho mwaka jana, mapato yao yaliongezeka kwa asilimia 40, huku baadhi ya watoto wakirejea shuleni na wanawake kupata mitaji.



Leave a Reply