Global Publishers
August 29, 2026
438 views
0 Comments

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumpa dhamana ya kuwa msaidizi wake wa kwanza, akiahidi kutekeleza majukumu yake kwa utii, uadilifu, uzalendo na uchapakazi.
Ndejembi ametoa kauli hiyo leo, Agosti 29, 2026, wakati akizungumza na wananchi wa Jimbo la Chamwino waliojitokeza kwa wingi kumpokea nje ya Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma, muda mfupi baada ya kuapishwa kuwa Makamu wa Rais.

Amesema atatumia nafasi hiyo kumsaidia Rais Samia kwa uadilifu na kuhakikisha anawatumikia Watanzania wote bila ubaguzi, kwa lengo la kuchangia katika kuharakisha maendeleo ya nchi.
“Nitaendelea kufanya kazi ya kumsaidia Mheshimiwa Rais kwa uadilifu na kuwatumikia Watanzania wote ili kuharakisha maendeleo ya nchi yetu,” amesema Ndejembi.

Aidha, Makamu wa Rais amesema ataendelea kuwa mwakilishi mzuri wa vijana nchini na kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha Tanzania inaendelea kupiga hatua katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
Ndejembi ameapishwa leo katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Chamwino, baada ya kuthibitishwa na Bunge kwa asilimia 100 jana, Agosti 28, 2026.





