Vita kati ya binadamu na mbu imeingia hatua mpya, huku mbinu za zamani za kuwadhibiti zikikabiliwa na usugu wa viuatilifu na wanasayansi wakitafuta silaha mpya za kuzuia wadudu hao kueneza malaria, dengue na chikungunya.
Agosti 20 kila mwaka dunia huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mbu, ikiwa ni kumbukumbu ya ugunduzi wa Sir Ronald Ross mwaka 1897 kuhusu uhusiano kati ya mbu na maambukizi ya malaria.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mwaka 2024 kulikuwa na wagonjwa wa malaria milioni 282 na vifo 610,000 duniani kote.
Afrika ilibeba mzigo mkubwa zaidi wa ugonjwa huo, ikichangia asilimia 94 ya wagonjwa na asilimia 95 ya vifo, huku takribani watoto 438,000 wakifariki kutokana na malaria.
Katika vita hiyo, binadamu wamekuwa wakitumia silaha mbalimbali, ikiwemo vyandarua vilivyotiwa dawa, unyunyiziaji wa dawa ndani ya nyumba na udhibiti wa mazalia ya mbu.
WHO inapendekeza matumizi ya vyandarua vilivyotiwa dawa na unyunyiziaji wa dawa kwenye kuta za ndani za nyumba. Vyandarua humzuia mbu kumfikia mtu na vinaweza kumuua au kumdhoofisha anapogusana na dawa.
Tangu mwaka 2000, zaidi ya vyandarua bilioni tatu vimesambazwa katika nchi zilizoathirika na malaria.
Lakini vita hiyo haijawa rahisi. Mbu wameanza kujenga usugu dhidi ya baadhi ya viuatilifu, hasa pyrethroids, hali inayowalazimu wanasayansi kutafuta silaha mpya za kukabiliana nao.
Kwa mujibu wa WHO, usugu dhidi ya viuatilifu umeonekana katika nchi 48, hali inayoweza kupunguza ufanisi wa baadhi ya mbinu zinazotumika kuwadhibiti.
Moja ya majibu ya kisayansi ni matumizi ya vyandarua vyenye mchanganyiko wa dawa mbili, pyrethroid na chlorfenapyr, ambavyo tayari vimetumika katika nchi 17 za Afrika.
Utafiti mwingine unahusu mbu waliobadilishwa vinasaba, wakiwemo mbu dume wenye sifa zinazoweza kupunguza uwezo wao wa kuzaliana.
WHO inaunga mkono utafiti huo, lakini inasisitiza tathimini ya usalama wa afya, mazingira na ikolojia kabla ya teknolojia hizo kutumika kwa kiwango kikubwa.
Kwa magonjwa yanayoenezwa na mbu aina ya Aedes, wanasayansi wanachunguza pia matumizi ya bakteria aina ya Wolbachia, anayeingizwa kwenye mbu ili kupunguza uwezo wao wa kusambaza virusi.
Nchini Tanzania, vita hiyo inaendelea kwa kutumia mchanganyiko wa mbinu zinazolenga kuzuia mbu kuzaliana na kuwafikia binadamu.
Mtafiti Kiongozi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Kituo cha Amani kilichopo Muheza, Tanga, Dk William Kisinza, amesema hatua muhimu ni kuhakikisha maambukizi ya malaria yanazuiwa kwa kudhibiti mbu wanaoeneza ugonjwa huo.
Amesema njia za kuzuia mbu zimeainishwa na wataalamu wa afya na miongozo ya WHO, ikiwemo matumizi sahihi ya vyandarua vilivyowekwa dawa, hasa nyakati za usiku.
Amesema njia nyingine ni kupulizia dawa zenye mabaki ya muda mrefu kwenye kuta za ndani za nyumba, maarufu kama Indoor Residual Spraying (IRS).
“Njia nyingine ambayo hata Serikali ya Tanzania na nchi zingine zinaitumia ni viuadudu. Kuna tafiti zimeonyesha viuadudu ni mbinu sahihi zaidi, ambapo hapa nchini tuna kiwanda Kibaha,” amesema.
Ameongeza kuwa viuadudu vinaweza kutumika kwenye mazalia ya mbu na kuwaua kabla hawajafikia hatua ya kuwa mbu waliokomaa.
“Viuadudu vinaua kabla mbu hawajawa pevu. Hiyo maana yake wanaua lava, hayo ndiyo matumizi sahihi,” amesema.
Vita dhidi ya malaria havilengi mbu pekee. Binadamu pia wameanza kutumia chanjo kama silaha ya kupunguza madhara ya ugonjwa huo.
WHO imeidhinisha chanjo mbili za malaria, RTS,S na R21/Matrix-M, kwa matumizi kwa watoto wanaoishi katika maeneo yenye malaria.
Hata hivyo, WHO inasisitiza kuwa hakuna njia moja inayoweza kumaliza malaria.
Vyandarua, unyunyiziaji wa dawa, udhibiti wa mazalia, chanjo na mbinu nyingine zinapaswa kutumika kwa pamoja kulingana na mazingira na kiwango cha maambukizi.
Njia nyingine inayotumika ni IRS, ambapo dawa yenye mabaki ya muda mrefu hunyunyiziwa kwenye kuta za ndani za nyumba ili kuua au kuzuia mbu.
WHO pia imeanza kupendekeza matumizi ya spatial emanators, vifaa vinavyotoa kemikali hewani kwa lengo la kuzuia, kuvuruga au kuua mbu.
Udhibiti wa mazalia nao huhusisha kuondoa au kutibu maeneo yenye maji yanayoweza kuwa mazalia ya mbu.
Mbinu hizo zimeanza kuonyesha matokeo nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa tamko la Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe, lililotolewa Aprili 25, 2026, vifo vya malaria vilipungua kwa asilimia 50, kutoka 2,460 mwaka 2020 hadi 1,231 mwaka 2025.
Maambukizi katika jamii nayo yalishuka kutoka asilimia 8.1 mwaka 2022 hadi asilimia 5.7 mwaka 2025.
Wagonjwa waliothibitika kuwa na malaria katika vituo vya afya wamepungua kwa zaidi ya nusu, kutoka milioni sita mwaka 2020 hadi milioni 2.8 mwaka 2025.
Serikali ilitenga Sh20 bilioni katika mwaka wa fedha 2024/25 na 2025/26 kwa ajili ya unyunyiziaji wa viuadudu vya kibaiolojia kwenye mazalia ya mbu.
Fedha hizo zimewezesha kununuliwa kwa lita 1.25 milioni za viuadudu vilivyosambazwa katika halmashauri zote 184.
Mapambano hayo yamepewa msukumo zaidi kupitia Mpango Mkakati wa Taifa wa Malaria wa 2026–2030, unaoweka mkazo katika kuzuia maambukizi, kudhibiti mbu na kuhakikisha wagonjwa wanapimwa na kutibiwa kwa wakati.
Dk Magembe amesisitiza umuhimu wa ushiriki wa jamii katika kufikia lengo la kutokomeza malaria ifikapo mwaka 2030.


